McEddy Elroy

Friday, February 25, 2011

MWAKALEBELA APANGUA KESI YA KWANZA MAHAKAMANI

ALIYEKUWA mshindi wa kwanza katika kura za maoni nafasi ya ubunge wa Iringa Mjini (CCM),Frederick Mwakalebela (41),ameanza kupangua kesi za kutoa hongo kwenye mchakato wa kura za maoni zinazomkabili baada ya kesi ya kwanza dhidi yake, kuondolewa mahakamani.

Aidha, mahakama ya wilaya ilimwachia huru Mwakalebela kwenye kesi namba 4 ya mwaka 2010 iliyokuwa inamkabili lakini hata hivyo, mahakama hiyo haikufuta mashitaka dhidi yake.

Mwakalebela sasa anaelekeza nguvu kwenye kesi namba 8 pia ya mwaka 2010 ambayo inamkabili yeye pamoja na mkewe,Selina, ambayo ipo hatua ya kutolea hukumu pingamizi la kisheria iwapo iondolewa mahakamani au la na kwamba itafikishwa mahakama ya Mkoa wa Iringa,Jumatatu ya Februari 28,mwaka huu.

Hakimu wa mahakama ya wilaya,Festo Lwila aliyekuwa anasikiliza shauri namba 4 dhidi ya Mwakalebela ameondoa kesi hiyo mahakamani na kumwachia huru mtuhumiwa huyo baada ya kuridhika na hoja moja ya upande wa utetezi kwamba kulikuwa na mapungufu ya kisheria kwenye hati ya mashitaka.

Mapungufu hayo ni mtuhumiwa kushitakiwa kwa makosa mawili kwenye hati moja ya mashitaka na hivyo kumfanya mtuhumiwa ashindwe kuelewa kwa usahihi kosa linalomkabili kitu ambacho kinaweza kumfanya ashindwe kuandaa utetezi wake.

Awali,upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Basil Mkwata wa Mkwata Law Chambers,uliwasilisha pingamizi la awali la kisheria mahakamani hapo ambalo lilikuwa na hoja tatu.

Hoja hizo ni pamoja na kifungu namba 15 (1) b cha sheria namba 11 ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 alichoshitakiwa nacho mtuhumiwa kilikuwa kinawahusu zaidi watumishi au wanaoshikilia ofisi za umma.

Hoja ya pili ilikuwa kwamba, kifungu Na. 21 (1) ( a) na 24 (8) ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010, hakitengenezi kosa kwa sababu vinazungumzia mwenendo usiofaa (unfair Conduct) kwenye kampeni za uchaguzi.

Wakili Mkwata katika hoja yake hiyo alisema katika sheria ya gharama za uchaguzi,hakuna hata sehemu moja iliposema waziwazi kwamba Unfair Conduct ni kosa la jinai na kwamba ni suala ambalo linaweza kutatuliwa nje ya mahakama ikiwemo mtuhumiwa wa Unfair Conduct kuenguliwa kwenye nafasi anayogombea.

Hoja ya tatu ni kwamba hati ya mashitaka haikuandaliwa vyema kwa kugumbukwa na mapungufu ya kisheria hususani kumshitaki mtuhumiwa kwa makosa mawili kwa kutumia sheria mbili tofauti kwenye hati moja ya mashitaka.

Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo,hakimu Lwila alizitumpilia mbali hoja ya kwanza na ya pili lakini akakubaliana na upande wa utetezi kwenye hoja ya tatu.

Alisema kitendo cha upande wa mashitaka kumshitaki mtuhumiwa kwa makosa mawili kwenye hati moja ya mashitaka ni kinyume cha sheria kwani mtuhumiwa anaweza asifahamu kwa ufasaha kosa linalomkabili na hivyo kushindwa kuandaa utetezi wake kwa hiyo alimwachia huru Mwakalebela.

“Mshitakiwa anakuwa huru na upande wa mashitaka una hiari, kama bado una-Interest na shauri hili walete upya mahakamani hati nyingine ya mashitaka kwa kuzingatia sheria.
Umati mkubwa uliofurika mahakamani ulionekana kufurahia uamuzi huo na kumfuata Mwakalebela kumpongeza mara baada ya kuteremka kizimbani.

Hata hivyo,Mwakalebela mwenyewe aligoma kuzungumza na waandishi wa habari kwa maelezo kuwa hawezi kuzungumza kwa sababu bado anakabiliwa na kesi nyingine ambayo itarejeshwa mahakama ya Mkoa wa Iringa,Jumatatu ijayo.

Upande wake,Mwendesha mashitaka wa Takukuru Mkoa wa Iringa,Imani Nitume aliwataka wandishi wa habari kuwa na subira na kwamba watajulishwa uamuzi wa Takukuru baada ya hukumu hiyo.
“Jamani haya ni mambo ya kiofisi msubiri tutawaambia hatua tutakazochukua lakini hata hivyo si mmesikia wenyewe,uamuzi wa mahakama ni mzuri na umenyooka,” alisema Nitume.

Mwakalebela alishitakiwa mahamakani hapo kwa madai kuwa, mwezi Juni mwaka huu, katika kijiji cha Mkoga Manispaa ya Iringa alitoa hongo ya Sh.100,000 kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamisi Luhanga ili azigawe kwa wapiga kura 30 wa CCM ili wampigie kura za maoni zilizofanyika Agosti mosi, mwaka huu.

Kuondolewa kwa kesi hiyo mahakamani,inamaanisha kuwa Takukuru wamepata pigo lingine baada ya kesi iliyokuwa inamkabili Waziri wa zamani Joseph Mungai na viongozi wengine wa CCM wawili ya kutoa hongo kwenye mchakato wa kura za maoni pia kuondolewa mahakamani, mwezi Januari,mwaka huu.

Mungai (66) pamoja na Katibu wa Umoja wa vijana wa CCM wa Wilaya ya Mufindi, Fidel Cholela (39) na Moses Masasi walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 15 ya rushwa kwenye mchakato wa kura za maoni kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010 .

Hata hivyo,mwezi uliopita,hakimu Mary Senapee wa mahakama ya Mkoa wa Iringa aliyekuwa anasikiliza shauri la Mungai na wenzake aliliondoa mahakamani shauri hilo baada ya kuridhika na hoja za utetezi lakini akasema Takukuru wako huru kufungua kesi upya kwa kufuata sheria zilizopo.

Alipohojiwa,Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa,Emma Kuhanga alisema kilichofanyika mahakamani si kumfutia mashtaka Mungai na wenzake bali kuondoa kesi mahakamani na kwamba Takukuru wako huru kufungua upya mashtaka.

Alisema tayari wameshapeleka kusudio la kufungua upya mashtaka ambalo lilipelekwa Mahakama Kuu tangu Februari Mosi, mwaka huu.

“Kwa hiyo kinachofanyika hivi sasa ni kupitia hukumu ya mahakama, kupitia upya jalada la kesi ili tufungue upya kesi dhidi ya Mungai na wenzake, tukishafungua tutawapeni taarifa,” alisema Kuhanga.

1 comment: