Viti vipya vya bunge
Bunge la Kenya lililokarabatiwa na
ambalo limekuwa gumzo kubwa kwa sababu ya gharama ya viti vya bunge hilo,
hatimaye limefunguliwa rasmi na rais wa nchi hiyo Mwai Kibaki.
Viti hivyo vimegharimu dola 3,000 za
kimarekani kwa kila kiti kimoja vikiwa jumla ya 350 vimetengenezwa na kitengo
cha magereza nchini humo.
Zabuni ya kwanza ya kutengeneza viti
hivyo ilitolewa kwa kampuni moja ya nje lakini ilifutwa baada ya baadhi ya
wabunge kugundua kila kiti kingegharimu dola 5000 za kimarekani.
Maafisa wanasema ukarabati huo
uliogharimu dola milioni 12 utaliweka bunge katika mfumo mpya wa kisasa wa
komputa.
"Mabadiliko tunayoyafanya
yataleta mabadiliko chanya katika uongozi," spika wa bunge Kenneth Marende
ameiambia BBC.
Amesema mfumo wa kupiga kura wa
elektroniki utawawezesha wabunge kupiga kura kwa uhuru wao binafsi kuliko
kulazimika kupiga kura kwa kuhofia vyama vyao.
"sasa mbunge atakuwa peke yake,
huru kabisa binafsi, atafanya maamuzi yake na kubonyeza tu kitufe."
Mwandishi wa BBC Odeo Sirari mjini
Nairobi, anasema baadhi wanaona viti hivyo kuwa ni vya gharama kubwa sana
kuliko mabunge mengine katika jumuiya ya madola.
Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na
rais Mwai Kibaki pamoja na wabunge ni miongoni mwa wanaolipwa mshahara wa juu
sana barani Africa.
Wabunge walifurika katika jengo hilo
lililokarabatiwa wakati rais na spika wakiongoza utaratibu wa sherehe za
ufunguzi.
Ukarabati huo ulianza mwezi Aprili
mwaka 2010 na ulikuwa umepangwa kuchukua mwaka mmoja kumalizika lakini
ulichelewa kwasababu ya utata ulioghubika zabuni yake, mwandishi wetu anasema.
Bunge la zamani
Mbunge John Mbadi, katika kamati ya
uwekezaji aliongoza upinzani juu ya zabuni ya kwanza.
"hatukuweza kuelewa ni kwa vipi
wabunge wangekuwa wanakaa katika viti vinavyogharimu karibu shilingi 400,000 za
Kenya kama dola 5,000, ambazo kwa kiwango chochote cha kawaida zingeweza
kujenga nyumba kwa wananchi kadhaa," ameiambia BBC.
"ilikuwa ni upuuzi,"
amesema.
Mwandishi wetu anasema watu wengi
wamelalamika kuwa gharama za sasa bado ni juu.
David Langat, anayesimamia
uzalishaji katika magereza nchini Kenya, amesema vifaa vyote vilivyotumika
vilitoka nchini Kenya lakini gharama za viti zimekuwa kubwa sana.
Ameiambia BBC kuwa viti hivyo vyenye
uzito wa kilo 50 kila kimoja vina kinga dhidi ya moto na vina dhamana ya miaka
30.
Kwa sasa Kenya ina jumla ya wabunge
220 lakini ukumbi huo umewekwa viti 350 idadi ambayo watachaguliwa katika
uchaguzi ujao mwezi Machi kwa mujibu wa katiba mpya.