McEddy Elroy

Tuesday, July 20, 2010

MAKADA WA CCM WAKANYAGANA UBUNGE IRINGA

Julai 20:HARAKATI za kuwania ubunge zinaonekana kuwa kali baada ya makada 58 kuchukua fomu za kuwania ubunge kupitia CCM kwenye majimbo nane ya Mkoa wa Iringa, mpaka jana ,Julai 19.

Takwimu zilizopatika zinaonesha kuwa, majimbo yanayoongoza kwa kuwa na wagombea wengi ni Kalenga-Iringa vijijini makada 13, Iringa Mjini makada 12, Njombe Kaskazini 11, Njombe Magharibi tisa, Makete wanne, Kilolo watatu, Mufindi Kaskazini watatu na Njombe Kusini wawili.

Ushindani mkali unaonesha kuwa katika jimbo la Manispaa ya Iringa lililokuwa linashikiliwa na Monica Mbega na Njombe Kaskazini ambalo lilikuwa likishikiliwa na Jackso Makweta.

Mpaka jana jumatatu julai 19, Mwenyekiti wa CCm Mkoa wa Iringa,Deo Sanga, maaru kama Jah People pia alichukua fomu kupambana na mbunge huyo wa siku nyingi,Jackson Makweta.

Katibu wa CCM wilaya ya Njombe Osea Mpagike aliwataja wengine wanaowania jimbo la Njombe Kaskazini kuwa ni Musa Mgata, Dickson Mtikwa, Jackson Makweta, Alatanga Nyagawa, Martin Chodota, Joachim Kinyunyu, Lena Hongeli, Laula Malecela, Onesmo Kinine na Julius Ngeme.

Kwa upande wa Jimbo la Iringa mjini, wanaoinyemelea ni Frederick Mwakalebela, Ado Mwasongwe, Fadhili Ngajilo, Yahya Msigwa, Jesca Msambatavangu, Thomas Kimata, Dkt. Kalinga, Monica Mbega, John Kiteve, Ben Mpete, Cherestino Mofuga na Zuberi Mwachura.

Kaimu Katibu CCM wilaya ya Iringa ambaye ni Katibu wa vijana, Pius Seleman alisema waliochukua fomu katika jimbo la Isimani ni Festo Kiswaga na Yahya Mtete wakati William Lukuvi anatarajia kuchukua siku ya mwisho na kuirudisha.

Alisema Jimbo la Kalenga ni Bruceson Kibasa, Abbas Kandoro, Anjero Mbunda, Stanslaus Mhongole, Anejlus Kisiga, Dkt. William Mgimwa, Victor Masangula, Hafsa Mtasiwa, Edward Mtakimwa, Richard Mfalingundi, Gabriel Kalinga, George Mlawa, Anset Sambala na Leonard Mwalu wakati kwa upande wa Jimbo la kilolo ni Profesa Peter Msola, Stephen Mwaduma na Venance Mwamoto ambao wote wamewahi kushika nafasi hiyo kwa vipindi tofauti.

Jimbo la Mufindi Kaskazini ni Jeseph Mungai, Mahamud Mgimwa, na Alamu Mwawaya na kwa upande wa Jimbo la Makete ni Benedict Mahenge, Amalaki Ngajilo, Zilumba Sanga, Anna Luvanda na Norman Sigalla.Jimbo la Njombe Kusini ni Anna Makinda na Demist Msemwa, jimbo la Njombe Magharibi ni Yono Kevela, Isaya Manjele, Japhet Mlagala, Graham Ngela, Thomas Nyimbo, Solomoni Nongono, June Ngole, Geison Lenge na Yahya Chaula.

Mwisho wa kurudisha fomu za kuwania kuteuliwa nafasi hiyo ni kesho jumatano, julai 21 ambapo itajulikana na ni makada wangapi wameingia katika kinyang’anyiro hicho.

Sunday, July 18, 2010

MZIMU WA KADI FEKI WAENDELEA KUITESA CCM

Julai01:MZIMU wa kadi feki umeendelea kukiandama Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kadi kumi kukamatwa katika Jimbo la Isimani na Kalenga Mkoani hapa zikidawa kuingizwa majimboni humo na makada wa CCM walioonesha nia ya kuwania majimbo hayo.

Taarifa za kuaminika zinasema kuwa, katika jimbo la Isimani ambalo mbunge wake wa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam,William Lukuvi zimekamatwa kadi saba wakati Kalenga ambako mbunge wake ni Stephen Galinoma,zimekamatwa kadi tatu.

Katibu wa CCM wilaya ya Iringa vijijini,Luciano Mbossa amethibitisha kukamatwa kwa kadi hizo na kueleza kuwa endapo itathibitishwa, wale wote waliohusika watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa katiba na kanuni za adhabu za CCM.

Inadaiwa kuwa kadi zilizokamatwa jimbo la Isimani alikutwa nazo Katibu wa CCM tawi la Maperamengi ambaye anadaiwa kuwa ni mfuasi mkubwa wa kada mmoja wa chama hicho,Leonard Mwalu maarufu kama Amazoni ambaye ameonesha nia ya kupambana na Lukuvi katika jimbo hilo.

Amazoni mwenyewe alipotafutwa hakukanusha wala kukubali bali alisema hakuwa na nafasi ya kuzungumza na mwandishi wa habari hizi kwa madai kuwa alikuwa anaendesha gari na kuomba apigiwe baada ya saa moja,ingawa baadaye simu yake haikupatikana tena.

Uchunguzi unaonesha kuwa, namba za kadi zinazodaiwa kukutwa kwa Katibu huyo wa CCM wa tawi la maperamengi ni AD 3709780, AD 3709781, AD 3709782, AD 3709783, AD 3709784, AD 3709785 na AD 3709786.

Kwa upande wa Kalenga,kadi tatu feki zinadaiwa kukutwa kwa Katibu wa Uchumi na Mipango kata ya Kiponzero,Jordan Kisinini ambaye anadaiwa ni mfuasi mkubwa wa mmoja wa makada walioonesha nia ya kuwania jimbo la Kalenga ambaye pia ni mmoja wa Wakurugenzi wa Benki Kuu (BoT),Dk.William Mgimwa.

Namba za kadi hizo ni AD 3055654, AD 3055655 na AD 3055656 na kwamba Kisinini alikanusha kukutwa na kadi hizo ingawa muhtasari wa kikao cha tawi la CCM Kiponzero wa kushughulikia suala hilo unaonesha kuwa Kisinini alikiri kupokea kadi hizo kutoka kwa Katibu wa CCM Kata ya Maboga,Erick Kahwanga ingawa naye alikanusha kutoa kadi hizo.

Dk.Mgimwa kwa upande wake alikiri kusikia habari za mtu mmoja katika Jimbo la Kalenga kukamatwa na kadi feki lakini alikanusha vikali kuhusika na kadi hizo na kueleza kuwa hizo ni njama za wapinzani wake kumchafua kisiasa.

Kumekuwepo na madai kwamba baadhi ya makada wa CCM wanaotaka kuwania jimbo la Kalenga na Isimani, wamemwaga kadi feki ili kuongeza idadi ya wanachama watakaowapigia kura katika zoezi la kura za maoni kupata mgombea wa jimbo.

Katibu wa CCM wilaya hiyo,Mbossa anakiri kuwepo madai hayo na kueleza kuwa mpaka sasa kadi halali zilizogawiwa katika majimbo hayo mawili ni zaidi ya 9000 na kwamba ameandaa ziara ya kukagua uandikishaji na uingizaji wanachama wapya katika daftari kwenye matawi yote ya majimbo hayo ili kubaini kadi hizo feki.

“Baada ya ziara hii, nitajua kwa ufasaha makatibu wa matawi waliohusiaka kuingiza wanachama wapya kwa kutumia kadi feki na hatua kali dhidi yao na waliotoa kadi hizo zitachukuliwa,” alisema Mbossa.

Mwisho.