Julai01:MZIMU wa kadi feki umeendelea kukiandama Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kadi kumi kukamatwa katika Jimbo la Isimani na Kalenga Mkoani hapa zikidawa kuingizwa majimboni humo na makada wa CCM walioonesha nia ya kuwania majimbo hayo.
Taarifa za kuaminika zinasema kuwa, katika jimbo la Isimani ambalo mbunge wake wa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam,William Lukuvi zimekamatwa kadi saba wakati Kalenga ambako mbunge wake ni Stephen Galinoma,zimekamatwa kadi tatu.
Katibu wa CCM wilaya ya Iringa vijijini,Luciano Mbossa amethibitisha kukamatwa kwa kadi hizo na kueleza kuwa endapo itathibitishwa, wale wote waliohusika watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa katiba na kanuni za adhabu za CCM.
Inadaiwa kuwa kadi zilizokamatwa jimbo la Isimani alikutwa nazo Katibu wa CCM tawi la Maperamengi ambaye anadaiwa kuwa ni mfuasi mkubwa wa kada mmoja wa chama hicho,Leonard Mwalu maarufu kama Amazoni ambaye ameonesha nia ya kupambana na Lukuvi katika jimbo hilo.
Amazoni mwenyewe alipotafutwa hakukanusha wala kukubali bali alisema hakuwa na nafasi ya kuzungumza na mwandishi wa habari hizi kwa madai kuwa alikuwa anaendesha gari na kuomba apigiwe baada ya saa moja,ingawa baadaye simu yake haikupatikana tena.
Uchunguzi unaonesha kuwa, namba za kadi zinazodaiwa kukutwa kwa Katibu huyo wa CCM wa tawi la maperamengi ni AD 3709780, AD 3709781, AD 3709782, AD 3709783, AD 3709784, AD 3709785 na AD 3709786.
Kwa upande wa Kalenga,kadi tatu feki zinadaiwa kukutwa kwa Katibu wa Uchumi na Mipango kata ya Kiponzero,Jordan Kisinini ambaye anadaiwa ni mfuasi mkubwa wa mmoja wa makada walioonesha nia ya kuwania jimbo la Kalenga ambaye pia ni mmoja wa Wakurugenzi wa Benki Kuu (BoT),Dk.William Mgimwa.
Namba za kadi hizo ni AD 3055654, AD 3055655 na AD 3055656 na kwamba Kisinini alikanusha kukutwa na kadi hizo ingawa muhtasari wa kikao cha tawi la CCM Kiponzero wa kushughulikia suala hilo unaonesha kuwa Kisinini alikiri kupokea kadi hizo kutoka kwa Katibu wa CCM Kata ya Maboga,Erick Kahwanga ingawa naye alikanusha kutoa kadi hizo.
Dk.Mgimwa kwa upande wake alikiri kusikia habari za mtu mmoja katika Jimbo la Kalenga kukamatwa na kadi feki lakini alikanusha vikali kuhusika na kadi hizo na kueleza kuwa hizo ni njama za wapinzani wake kumchafua kisiasa.
Kumekuwepo na madai kwamba baadhi ya makada wa CCM wanaotaka kuwania jimbo la Kalenga na Isimani, wamemwaga kadi feki ili kuongeza idadi ya wanachama watakaowapigia kura katika zoezi la kura za maoni kupata mgombea wa jimbo.
Katibu wa CCM wilaya hiyo,Mbossa anakiri kuwepo madai hayo na kueleza kuwa mpaka sasa kadi halali zilizogawiwa katika majimbo hayo mawili ni zaidi ya 9000 na kwamba ameandaa ziara ya kukagua uandikishaji na uingizaji wanachama wapya katika daftari kwenye matawi yote ya majimbo hayo ili kubaini kadi hizo feki.
“Baada ya ziara hii, nitajua kwa ufasaha makatibu wa matawi waliohusiaka kuingiza wanachama wapya kwa kutumia kadi feki na hatua kali dhidi yao na waliotoa kadi hizo zitachukuliwa,” alisema Mbossa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment