McEddy Elroy

Showing posts with label Uchaguzi 2010. Show all posts
Showing posts with label Uchaguzi 2010. Show all posts

Tuesday, October 5, 2010

TUNADI SERA ZETU

Wagombea ubunge katika jimbo la Kalenga Mkoani Iringa kutoka kushoto na vyama vyao kwenye mabano ni John Katindasa (TLP), Rehema Makoga (Chadema) na Ismail Makuke (Jahazi Asilia) wakijibu maswali ya wapiga kura katika mdahalo wa wagombea na wapiga kura wa jimbo hilo uliofanyika kwenye ukumbi wa serikali ya kijiji.Mgombea wa CCM,Dk.William Mgimwa hakuwepo kwenye mdahalo kutokana marufuku ya CCM kwa wagombea wa ngazi zote kuhudhuria midahalo.

MGOMBEA WA UBUNGE KALENGA KUPITIA TLP AKIWA HANA LA KUFANYA

Mgombea wa Ubunge Jimbo la Kalenga,kupitia Chama cha TLP,John Katindasa (Mwenye suti nyeusi katikati) akiwa hana la kufanya baada ya gari lake kugoma kuwaka muda mfupi baada ya kumalizika kwa mdahalo wa wagombea na wapiga kura wa Jimbo la Kalenga.Wengine walioshiriki mdahalo huo ni Mgombea wa kupitia Chadema, Rehema Makoga na mgombea kutia Jahazi Asilia,Ismail Makuke.

Wednesday, September 22, 2010

MWAKALEBELA KATIKA MATUKIO TOFAUTI NA KIKWETE SAMORA JANA

Aliyeongoza katika kura za maoni,Frederick Mwakalebela jana katika uwanja wa Samora alishangiliwa kuliko hata Kikwete hali iliyoonesha dhahiri kwamba ni kipenzi cha wakati wa Jimbo la Iringa Mjini.Picha tatu tofauti zinaonesha Kikwete akimnadi Mwakalebelas katika ile hali ya kuvunja makundi na kutangaza rasmi kwamba anakiunga mkono Chama Cha Mapinduzi pamoja na mgombea wa Jimbo la Iringa Mjini,kupitia chama hicho,Monica Mbega.

Wednesday, September 15, 2010

Wednesday, September 8, 2010

JK ALIPOKUWA MORO


NCCR-MAGEUZI IRINGA KIKAAONGONI

MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Iringa Mjini,Theresia Mahongo amekitaka Chama cha NCCR-Mageuzi kuitisha mkutano wa hadhara kuwaomba radhi mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kupitia Chadema,Mchungaji Peter Msigwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,Chiku Abwao.

NCCR-Mageuzi pia imetakiwa kuandika barua ya kuwaomba radhi Mchugaji Msigwa na Abwao na nakala yake kutumwa kwa Msimamizi huyo wa Uchaguzi Jimbo la Iringa Mjini.

Agizo hilo la Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Iringa kwa Chama cha NCCR-mageuzi limekuja siku tano baada ya wafuasi wa Mgombea wa Ubunge jimbo hilo kupitia Chama hicho cha NCCR-Mageuzi,Mariam Mwakingwe, kupanda jukwaani na kurusha matusi yasiyoandika katika mkutano wa kampeni uliofanyika Stendi ya Mabasi,Mjini Iringa,Agosti 31,mwaka huu.

Wafuasi hao ni Francis Blanka ambaye ni Katibu Mwenezi wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Mkoa wa Iringa na Benny Kapwani ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Iringa, kwa nyakati tofauti katika mkutano huo wa kampeni walipanda jukwaani na kuvurumisha matusi yasiyoandikika kwa mchungaji Msigwa na Abwao.

Kwa mujibu wa barua ya Mahongo ya Septemba 06,mwaka huu, kwenda kwa NCCR-Mageuzi ambayo Nipashe imepata nakala yake, Msimamizi huyo pia amekiagiza Chama hicho kuacha kumpeni za matusi vinginevyo kitatozwa faini ya Sh.100,000 au kufutwa kwenye kampeni hadi Oktoba 31,mwaka huu.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 5:8 (a) cha maadili ya Uchaguzi, (NCCR) mnaagizwa kuomba radhi hadharani katika eneo lilelile mlilotumia kutoa lugha ya kashfa. Mnaagizwa kutuletea tarehe utakayofanya mkutano huo wa kuomba radhi ndani ya siku tatu ili Kamati ya Maadili ya Uchaguzi uhudhurie kwa ajili ya kujiridhisha,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Maagizo hayo kwa NCCR-Mageuzi yaliyotolewa na Msimamizi huyo wa Uchaguzi,yanafuatia kikao cha Maadili ya Uchaguzi kilichoketi Septemaba 04,mwaka huu kujadili malalamiko yaliyowasilishwa kwenye kamati hiyo na Mchugaji Msigwa pamoja na Abwao.

Barua ya malalamiko hayo iliyosainiwa na Katibu wa Chadema Iringa Mjini,Suzane Mgonakulima, iliitaka ofisi ya Msimamizi huyo kuchukua hatua mara moja kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa ili kuepusha uvunjifu wa amani katika Jimbo hilo.

Katibu wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Iringa,James Mwamgiga amekiri kupokea barua ya msimamizi huyo lakini amesema hawataitekeleza na badala yake wamekata rufaa.

“Barua ile imekuja tofauti na tulivyokubalina kwenye kikao cha maadili, kuna maneno yameongezwa ikiwemo kuwaandikia (Mchungaji Msigwa na Abwao) barua ya kuwaomba radhi,..tunasubiri kwanza maamuzi ya rufani yetu,” alisema Mwamgiga.

Mwisho.

Wednesday, September 1, 2010

WAPINZANI IRINGA WAWEKA KANDO KAMPENI,WAANZA VITA YA MATUSI

Septemba 01:BAADHI ya wakazi wa Jimbo la Iringa mjini wamelaani vikali vitengo vya baadhi ya wafuasi wa wagombea wa ubunge wa jimbo hilo kuanza kampeni chafu za kurushiana matusi majukwaani.

Wananchi hao pia wametoa masikitiko na kuonyesha wasiwasi kama wafuasi hao wana nia njema na Jimbo hilo kutokana na kuacha kazi ya kueleza mikakati ya namna gani nzuri watakavyowahudumia wananchi na kutumia muda mrefu kutukanana.

Aidha, wananchi hao wamefikia hatua ya kuwalaani baada ya wafuasi wa Mgombea wa Ubunge Jimbo la Iringa Mjini kupitia unaojiita ‘Muungano wa Upinzani’, Mariam Mwakingwe kupanda jukwaani na kuanza kurusha matusi katika mkutano wa kampeni,Jumanne, Agosti 31,mwaka huu katika Stendi ya Mkoa wa Iringa.

Francis Blanka ambaye ni Katibu Mwenezi wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Mkoa wa Iringa na Benny Kapwani ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chma cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Iringa, kwa nyakati tofauti jana walipanda jukwaani na kuvurumisha matusi yasiyoandikika.

Walikuwa wanamshambulia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA,Chiku Abwao, ambaye katika uzinduzi rasmi wa kampeni za CHADEMA Mkoa wa Iringa, alidai kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wao (CHADEMA) Mkoa wa Iringa alijiuzulu wadhifa huo baada ya chake chake kubaini kuwa amenunuliwa na CCM ili kuwahujumu.

Mwingine aliyekuwa akiporomoshewa matusi hayo ni mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kupitia CHADEMA,Mchungaji Peter Msigwa
Chiku alidai kuwa,wanazo taarifa kwamba Kapwani ambaye alikuwa amechukua fomu za kuwania ubunge Jimbo la Isimani hakurejesha fomu hizo kutokana na kununuliwa na mgombea mwingine ambaye amekuwa Mbunge wa Isimani kwa miaka 15 na ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam,William Lukuvi,hivyo mgombea huyo wa CCM kupita bila kupingwa.

Ndipo vurugu zilipoanza ambapo jana Kapwani na Blanka walishirikiana kurusha matusi hayo kwa Abwao na Msigwa na kufanya baadhi ya watu waamini kuwa huenda watu hao walikuwa ‘wamechanganyikiwa’.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walisema wamesikitishwa na hali hiyo na kuitaka Serikali kupitia ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwaonya watu hao kama si kuwafuta kabisa kwenye kampeni.

“Tulikuja kusikia sera zao lakini kama tungejua kwamba tunakuja kusikia watu na heshima zao wakitukana hadharani wala tusingepoteza muda wetu,” alisema mkazi wa Ilala iliyetambulisha kwa jina la Elisha Mhanga.

Chiku Abwao mwenyewe aliiambia Blog hii baadaye kuwa alikuwa anakusanya ushahidi ili awasilishe kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Iringa Mjini kabla ya kufungua kesi mahakamani kwa sababu wazungumzaji walimshambulia yeye binafsi na biashara zake.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo,Theresia Mahongo alisema hakuwa amepata malalamiko yoyote lakini akavikumbusha vyama vya siasa kuzingatia maadili ya Uchaguzi waliyosaini vinginevyo watashughulikiwa.

“Binafsi sikuyasikia hayo matusi kwa sababu sikuwepo kwenye mkutano wao lakini nitafuatilia ili niwakumbushe kwamba kampeni siyo njia ya kuchochea uvunjifu wa mshikamano na amani tuliyonayo,” alisema Mahongo.

Umeibuka mpasuko mkubwa katika kambi ya upinzani Mjini Iringa mpasuko ambao ni dhahiri unaweza kumnufaisha mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kupitia CCM,Monica Mbega ambaye naye ana wakati mgumu kutokana na mpasuko ndani ya CCM katika Jimbo hilo unaodaiwa kuwepo baada ya aliyeongoza katika kura za maoni,Frederick Mwakalebela, kuenguliwa na NEC ya CCM.

Katika kambi ya upinzani,vyama vya TLP,CUF,APPT na NCCR-Mageuzi vinamuunga mkono mgombea kupitia NCCR-Mageuzi,Mariam Mwakingwe huku CHADEMA wakiwa hawautambui muungano huo hali ambayo imeleta uhasama mkubwa na kuanza kushambulia peupe kwenye majukwaa ya kampeni.

Mwisho

Monday, August 30, 2010

JK ANAPOGOMBANIWA NA WAPIGA KURA!


JK akigombaniwa na wapigakura huko Sumbawanga a.k.a Mjini Tupa uchawi

CHADEMA WAJINUFAISHA NA MGOGORO WA CCM

Agosti 30: CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Iringa jana (Agosti 30) kimezindua rasmi kampeni zake huku kikitumia mpasuko wa CCM katika Manispaa ya Iringa kama mtaji wake mkubwa.

CCM Manispaa ya Iringa kinadaiwa kuwa na mpasuko unaodaiwa kuwepo baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kumwengua Frederick Mwakalebela licha ya kuongoza katika kura za maoni na kumweka aliyeshika nafasi ya pili,Monica Mbega ambaye pia alikuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika viwanja vya Mwembetogwa, Manispaa ya Iringa, Mgombea wa CHADEMA,Mchugaji Peter Msigwa aliwaomba wanachama na wafuasi wa CCM kumkataa mgombea wa chama hicho,Monica Mbega kwa sababu siyo chaguo lao.

Msigwa huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa kampeni, alisema imekuwa ni kawaida kwa CCM kuwachagulia wananchi mgombea na kuwataka wananchi wa jimbo la Iringa Mjini kutodanganyika.

“Kwa niaba ya familia yangu na kwa niaba ya chama changu (CHADEMA), tunampa pole sana Mwakalebela kwa kuonewa na NEC ya CCM lakini tunawaomba wananchi wa Iringa, mfuteni machozi ndugu yetu huyu (Mwakalebela) kwa kuinyima kura CCM,” alisema Mchungaji Msigwa.

Mchungaji Msigwa ambaye uchaguzi wa mwaka 2005 aligombea jimbo hilo kupitia chama cha Tanzania Labour (TLP) alisema endapo atachaguliwa atawatumikia wananchi wa Manispaa ya Iringa kwa unyenyekevu mkubwa kwa sababu wao ndiyo waajiri wake.

Alisema atatumia vitivo mbalimbali vya Vyuo Vikuu vilivyopo Manispaa ya Iringa kuviunganisha na wananchi katika harakati ya kuvitumia Vyuo hivyo kuleta maendeleo.

Wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni pamoja na aliyekuwa kada wa CCM ambaye ametimkia CHADEMA na anagombea Jimbo la Njombe Kaskazini,Alatanga Nyagawa.

Nyagawa alijinasibu kuwa yeye, msigwa pamoja na aliyekuwa kada mwingine wa CCM aliyetimkia Chadema,Thomas Nyimbo tayari ni wabunge kutokana na kile alichokieleza kuwa wapinzania wao ni dhaifu.

“Tutatumia udhaifu wa wagombea wenzetu kushinda kwa kishindo,” alisema.

Moja ya udhaifu wa mgombea wa CCM katika jimbo la Njombe Kaskazini ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa Iringa,Deo Sanga maarufu Jah People,ni kudaiwa kuwa na elimu ya darasa la pili.

“Nitawaomba wananchi wa Njombe Kaskazini wamnyime kura Deo Sanga ili arudi MEMKWA (mpango maalum wa elimu kwa walioikosa),” alisema.

Hata hivyo,Sanga mwenyewe alipoongea na BLOG HII kwa simu alikanusha madai kwamba elimu yake ni darasa la pili bali akasema elimu yake ni darasa la saba na kwamba alisoma katika shule ya msingi Ikwega iliyopo wilayani Mufindi, ingawa alisema hakumbuki alihitimu mwaka gani.

“Mpaka nirejee kwenye kumbukumbu zangu ndiyo naweza kukueleza nilianza mwaka gani na nikamaliza mwaka gani,” alisema Deo Sanga, hata hivyo alipotafutwa baadaye alikuwa hapatikani.

Hata hivyo, alisema Nyagawa anayedai kwamba yeye (Sanga) ni mbumbumbu ni mfa maji anayetapatapa baada ya kuangushwa katika kura za maoni za CCM na kukumbilia CHADEMA.

Thursday, August 19, 2010

NIPENI TENA WANYALUKOLO 'BAYANGU'

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo,Prof.Peter Msolla (Kulia) akirejesha fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuomba kuwania tena jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. Anayepokea fomu hizo ni Msimamizi wa uchanguzi jimbo la Kilolo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo,Bosco Nduguru.

KIPYENGA CHAPULIZWA RASMI MAJIMBONI

Agosti 19:VIGOGO wawili wa CCM wa Mkoani Iringa waliotimkia Chadema,Alatanga Nyagawa na Thomas Nyimbo wamerejesha fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) za kuwania ubunge kwa tikiti ya chama hicho katika Majimbo ya Njombe Kaskazini na Njombe Magharibi.

Tofauti na Majimbo mengine, kama watapitishwa na NEC, watakaopambana Jimbo la Njombe kaskazini ni Deo Sanga, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa na Alatanga Nyagawa wa Chadema.

Aidha,Jimbo la Njombe Magharibi watakaopambana pia ni wawili tu ambao ni Thomas Nyimbo wa Chadema ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa tikiti ya CCM kwa kipindi cha miaka kumi ambaye atapambana Gelson Lwengwe wa CCM.

Kwa upande wa kilolo, Prof.Peter Msolla ambaye wakati akirejesha fomu mamia ya watu waliandama naye, atapambana na Cray Mwituka wa Chadema na mwana mama Mwaka Mgimwa wa chama cha Chausta.

“Nawashukuru wananchi kwa kuonesha imani kwangu na nitajihadi kuwahudumia vyema ili niwe mbunge wao wa kudumu kama wanavyoomba,” alisema Msolla ambaye alikuwa akijibu maombi ya wananchi waliokuwa wakiimba kutaka awe mbunge wao wa kudumu.

Wengine waliorejesha fomu hadi jana saa 9:00 alasiri ni kama ifuatavyo:

Mufindi Kusini.
Menrad Kingola (CCM).

Mufindi Kasikazini.
Mahamud Mgimwa (CCM) na Lawrance Mwabusi (NCCR-Mageuzi).

Jimbo la Kalenga.
Dr.William Mgimwa (CCM),Rehema Makoga (Chadema), Makuke Mginja (Jahazi Asilia) na John Lumuliko (TLP).

Jimbo la Isimani.
Benny Kapwani (Chadema), William Lukuvi (CCM) na Mussa Fufumbe (CUF).

Jimbo la Iringa Mjini.
Monica Mbega (CCM) na Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).

Mwisho.

Thursday, August 12, 2010

MAKADA WA CCM ZAIDI CORTIN, MWALIMU ANASWA KWA RUSHWA YA NGONO

Na Mawazo Malembeka

Agosti 12:MTUHUMIWA mwingine wa rushwa katika kura za maoni katika jimbo la Iringa Mjini,ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa,Fadhili Ngajilo, leo amepandishwa kizimbani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Ngajilo (31), ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu John cha Mjini Dodoma, alifikishwa mahakama ya Mkoa wa Iringa na kusomewa shitaka moja la kutoa hongo kinyume na sheria namba 11 ya kupambana na kuzuia rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010.

Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Consolatha Singano, Mwanasheria wa Takukuru,Prisca Mpepo alidai kuwa Ngajilo anadai kutoa hongo hiyo Julai 20,mwaka huu katika kijiji cha Mgongo,Manispaa ya Iringa.

Mwanasheria huyo alidai kuwa Ngajilo anadaiwa kutoa hongo ya Sh.30,000 kwa Kaimu Katibu wa CCM tawi la Mgogo,Gwido Sanga ili naye azigawe kwa wajumbe 30 wa CCM waliokuwa wamekusanyika kwenye nyumba ya Damas Mbilinyi kusubiri wagombea waliokuwa wanapita eneo hilo kujinadi.

Alidai kuwa hongo hiyo ililenga kuwashawishi wajumbe hao wampigie kura Ngajilo wakati wa kupiga kura za maoni.

Mtuhumiwa huyo alikana shtaka dhidi yake na Mwanasheria wa Takukuru, Prisca, alidai mahakamani hapo kwamba upelelezi haujakamilika na kwamba dhamana iko wazi kwa mtuhumiwa kama angetimiza masharti ambayo yangewekwa na mahakama hiyo.

Akisoma masharti ya dhamana kwa mtuhumiwa, hakimu Singano alisema mtuhumiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni wakazi wa Mkoa wa Iringa ambao pia wawe watumishi wa Serikali au taasisi yoyote inayotambulika kisheria na kwamba kila mdhamini asaini dhamana ya Sh.milioni mbili.

Hata hivyo, Ngajilo aliyekuwa anaonekana kujiamini muda wote wakati shaurio lake likisomwa, alikuwa ameandaa wadhamini wawili lakini mmoja ambaye alidaiwa kuwa ni baba yake alikataliwa na mahakama hiyo kwa kuwa nyaraka zake zilithibitisha kwamba siyo mtumishi wa serikali.

Hakimu Singano aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 06,mwaka huu, litakapotajwa tena na Ngajilo aliwekwa mahabusu wakati akisubiri kukamilisha taratibu za dhamana ambapo hadi majira saa saba mchana, alikuwa bado hajakamilisha taratibu hizo.

Watuhumiwa wengine kufikishwa mahakamani jana ni pamoja aliyewahi kuwa waziri kwa nyakati tofautitofauti na Mbunge wa siku nyingi wa jimbo la Mufindi Kaskazini,Joseph Munga akikabiliwa na makosa 15 ya rushwa.

Mwingine ni Frederick Mwakalebela ambaye licha ya kutokuwepo mahakama kwa taarifa, kesi yake ilifikishwa mahakamani na kusogezwa mbele hadi Agosti17,mwaka huu.

Wakati huo huo, Takukuru inamshikilia Mwalimu wa shule ya sekondari ya Pomerin iliyoko wilayani Kilolo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa,Michael Ngalingwa (35) kwa tuhuma ya kuomba na kupewa rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi wake wa kidato cha kwanza.

Taarifa zilizothibitishwa na Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa,Gasto Mkono, mwalimu huyo anadaiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza ili amsadie kufaulu vyema somo la kiingereza pamoja na kumpa ahadi ya kumsaidia matumizi madogomadogo awapo shuleni hapo.

Kwa mujibu wa Mkono, Takukuru walipewa taarifa za tukio hilo na wasamalia wema na kuweka mtego ulifanikiwa kumnasa mwalimu huyo kwenye moja ya nyumba za kulala wageni Mjini Iringa, saa sita ya usiku wa kuamkia leo (Agosti 12) akiwa na binti huyo.

Mkuu wa shule hiyo ya Pomerin, Shadrack Nyaulingo hakupatikana kwa maelezo kuwa alikuwa njia kwenda Takukuru kutoa baadhi ya taarifa muhimu zinazohusiana na tukio hilo.

Hata hivyo,msemaji mmoja wa Ofisi ya Dayosisi ya Iringa, (DIRA), ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa maelezo kuwa ofisi hiyo haihusiki na sula hilo kwa kuwa ni la binafsi zaidi (la Mwalimu aliyekamatwa) alikiri kuwepo kwa tukio hilo.

“Hata sisi tumepata taarifa hizi, ni kweli lakini naomba mtafute Mkuu wa shule atakueleza vyema, sisi (DIRA) hatuhusiki nalo kwa sababu ni la binafsi sana,” alisema kwa upole.

Mwisho

Wednesday, August 11, 2010

TAKUKURU IRINGA YAANZA KAZI,MUNGAI CORTINI

Agosti 11:TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo imeanza rasmi kuwapandisha kizimbani makada wa CCM waliotuhumiwa kutoa rushwa wakati wa kampeni za kura za maoni kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama hicho katika nafasi ya ubunge kwenye majimbo yao.

Waliokuwa wa mwanzo kuonja shubiri hiyo ya kupandishwa kizimbani ni pamoja na Mbunge wa Mufindi Kaskazini,Joseph Mungai na aliyeongoza kura za maoni jimbo la Iringa mjini,Frederick Mwakalebela.

Mungai (66), kwa pamoja na watu wengine wawili ambao ni pamoja na Katibu wa Umoja wa vijana wa CCM wa wilaya ya Mufindi,Fidel Cholela (39) na Moses Masasi wamefikishwa katika mahakama ya Mkoa wa Iringa wakikabiliwa na mashtaka 15 ya rushwa kinyume na sheria ya kuzuia na kupamna na rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010 .

Kwa upande wa Mwakalebela, shauri lake lenye tuhuma moja ya rushwa, limefikishwa katika mahakama hiyo ya Mkoa lakini limesongezwa mbele hadi Adosti 17,mwaka huu, kwa kuwa alikuwa na ruksa ya kutokuwepo mahakamani leo.

Mbele ya hakimu wa mahakama ya Mkoa wa Iringa,Merry Senapee, msoma mashtaka wa Takukuru,Prisca Mpepo alidai kuwa mnamo Julai 08,mwaka huu, katika kata ya Ihalimba, wilaya ya Mufindi, Mungai akiwa mmoja wa makada wa CCM waliokuwa wanawania kupitishwa katika kura za maoni kugombe ubunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini kwa pamoja na watuhumiwa wenzake, walitoa hongo ya Sh.10,000 kwa Mwenyekiti wa CCM tawi la Vikula kama kishawishi cha kumpigia kura wakati wa zoezi la kura za maoni.

Katika shtaka la pili, watuhumiwa wote kwa pamoja, siku na eneo hilo walitoa hongo ya Sh.10,000 kwa Konjesta Kiyeyeu ambaye alihudhuria kikao cha kamati ya CCM kijiji cha Vikula.

Msoma mashtaka aliendelea kudaia mahakamani hapo kuwa, katika shtaka la tatu, nne, tano na sita, watuhumiwa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.10,000/- kwa kila mmoja kwa Aldo Lugusi, Ezekiel Mhewa, Tulaigwa Kisinda na Jiston Mhagama kwa lengo hilihilo la kuwashawishi wampigie kura za maoni.

Shtaka la saba wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.20,000 kwa Maria Kihongosi na shtaka la nane kutoa hongo ya Sh.5,000 Lurent Mdalingwa wakati shtaka la tisa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.20,000 kwa Victory Kalinga ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kijiji cha Ugessa.

Katika mashtaka namba kumi hadi 12 washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa walitoa hongo ya Sh.2,000 kwa kila mmoja kwa Francis Chonya, Alfred Kisinga na Issac Tewele wakati shtaka la 13 wanadaiwa walitoa hongo ya Sh.10,000 kwa Sosten Kigahe.

Aidha, msoma mashtaka huyo alidai kuwa shitakana namba 14 watuhumiwa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.10,000 kwa Raphael Lutumo na shitaka la mwisho walitoa hongo ya Sh.20,000 kwa Andrew Mkiwa.

Watuhumiwa wote walikana mashtaka na hakimu Senapee alisema dhamana iko wazi kwa watuhumiwa kwa masharti kwamba kila mtuhumiwa awe na wadhamini wawili ambapo mmoja wa wadhamini hao awe anaishi Manispaa ya Iringa na kila mdhamini asaini bondi ya Sh.milioni tano.

Hadi wandishi wa habari hii wanatoka mahakamani majira ya saa tano asubuhi, si Mungai wala watuhumiwa wengine waliokuwa wametimiza masharti ya dhamana hivyo waliswekwa mahabusu ya mahakama wakisubiri jamaa zao kutimiza masharti ya dhamana.

Taarifa zilizopatikana baadaye majira ya saa 8.30 alasiri kutoka mahakamani hapo zilithibitisha kuwa watuhumiwa wote walitimiza masharti ya dhamana na kwamba shauri hilo litarejeshwa mahakamani hapo kwa kutajwa Agosti 25,mwaka huu.

Kwa upande wa shitaka lililofikishwa mahakamani hapo likimkabili Mwakalebela, lilidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa la rushwa Juni, mwaka huu, katika kijiji cha Mkoga,Manispaa ya Iringa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ya Takukuru,Mwakalebela anadaiwa kutoa hongo ya Sh.100,000 kwa Mwenyekiti wa CCM wa kijiji hicho,Hamisi Luhanga ili naye azigawe kwa wapiga kura wa CCM ambao wangempigia kura wakati wa zoezi la kura za maoni.

Mwakalebela alikuwa na udhuru hivyo shauri lake lilisongezwa mbele hadi Agosti 17,mwaka huu.

Hata hivyo, Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Iringa,Bonasian Kessy alisema Mwakalebela anashitakiwa kwa makosa mawili ya rushwa na kwamba shtaka lingine litafikishwa mahakamani kesho (Agosti 12) ingawa hakutaka kulifafanua.

Kamanda Kessy pia alithibitisha kuwa mtuhumiwa mwingine wa rushwa katika kampeni za kura za maoni ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa CCM Mkoa wa Iringa,Fadhili Ngajilo pia atapandishwa kizimbani kesho (Agosti 12) kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Mwisho.

Tuesday, July 20, 2010

MAKADA WA CCM WAKANYAGANA UBUNGE IRINGA

Julai 20:HARAKATI za kuwania ubunge zinaonekana kuwa kali baada ya makada 58 kuchukua fomu za kuwania ubunge kupitia CCM kwenye majimbo nane ya Mkoa wa Iringa, mpaka jana ,Julai 19.

Takwimu zilizopatika zinaonesha kuwa, majimbo yanayoongoza kwa kuwa na wagombea wengi ni Kalenga-Iringa vijijini makada 13, Iringa Mjini makada 12, Njombe Kaskazini 11, Njombe Magharibi tisa, Makete wanne, Kilolo watatu, Mufindi Kaskazini watatu na Njombe Kusini wawili.

Ushindani mkali unaonesha kuwa katika jimbo la Manispaa ya Iringa lililokuwa linashikiliwa na Monica Mbega na Njombe Kaskazini ambalo lilikuwa likishikiliwa na Jackso Makweta.

Mpaka jana jumatatu julai 19, Mwenyekiti wa CCm Mkoa wa Iringa,Deo Sanga, maaru kama Jah People pia alichukua fomu kupambana na mbunge huyo wa siku nyingi,Jackson Makweta.

Katibu wa CCM wilaya ya Njombe Osea Mpagike aliwataja wengine wanaowania jimbo la Njombe Kaskazini kuwa ni Musa Mgata, Dickson Mtikwa, Jackson Makweta, Alatanga Nyagawa, Martin Chodota, Joachim Kinyunyu, Lena Hongeli, Laula Malecela, Onesmo Kinine na Julius Ngeme.

Kwa upande wa Jimbo la Iringa mjini, wanaoinyemelea ni Frederick Mwakalebela, Ado Mwasongwe, Fadhili Ngajilo, Yahya Msigwa, Jesca Msambatavangu, Thomas Kimata, Dkt. Kalinga, Monica Mbega, John Kiteve, Ben Mpete, Cherestino Mofuga na Zuberi Mwachura.

Kaimu Katibu CCM wilaya ya Iringa ambaye ni Katibu wa vijana, Pius Seleman alisema waliochukua fomu katika jimbo la Isimani ni Festo Kiswaga na Yahya Mtete wakati William Lukuvi anatarajia kuchukua siku ya mwisho na kuirudisha.

Alisema Jimbo la Kalenga ni Bruceson Kibasa, Abbas Kandoro, Anjero Mbunda, Stanslaus Mhongole, Anejlus Kisiga, Dkt. William Mgimwa, Victor Masangula, Hafsa Mtasiwa, Edward Mtakimwa, Richard Mfalingundi, Gabriel Kalinga, George Mlawa, Anset Sambala na Leonard Mwalu wakati kwa upande wa Jimbo la kilolo ni Profesa Peter Msola, Stephen Mwaduma na Venance Mwamoto ambao wote wamewahi kushika nafasi hiyo kwa vipindi tofauti.

Jimbo la Mufindi Kaskazini ni Jeseph Mungai, Mahamud Mgimwa, na Alamu Mwawaya na kwa upande wa Jimbo la Makete ni Benedict Mahenge, Amalaki Ngajilo, Zilumba Sanga, Anna Luvanda na Norman Sigalla.Jimbo la Njombe Kusini ni Anna Makinda na Demist Msemwa, jimbo la Njombe Magharibi ni Yono Kevela, Isaya Manjele, Japhet Mlagala, Graham Ngela, Thomas Nyimbo, Solomoni Nongono, June Ngole, Geison Lenge na Yahya Chaula.

Mwisho wa kurudisha fomu za kuwania kuteuliwa nafasi hiyo ni kesho jumatano, julai 21 ambapo itajulikana na ni makada wangapi wameingia katika kinyang’anyiro hicho.