Monday, August 30, 2010

CHADEMA WAJINUFAISHA NA MGOGORO WA CCM

Agosti 30: CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Iringa jana (Agosti 30) kimezindua rasmi kampeni zake huku kikitumia mpasuko wa CCM katika Manispaa ya Iringa kama mtaji wake mkubwa.

CCM Manispaa ya Iringa kinadaiwa kuwa na mpasuko unaodaiwa kuwepo baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kumwengua Frederick Mwakalebela licha ya kuongoza katika kura za maoni na kumweka aliyeshika nafasi ya pili,Monica Mbega ambaye pia alikuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika viwanja vya Mwembetogwa, Manispaa ya Iringa, Mgombea wa CHADEMA,Mchugaji Peter Msigwa aliwaomba wanachama na wafuasi wa CCM kumkataa mgombea wa chama hicho,Monica Mbega kwa sababu siyo chaguo lao.

Msigwa huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa kampeni, alisema imekuwa ni kawaida kwa CCM kuwachagulia wananchi mgombea na kuwataka wananchi wa jimbo la Iringa Mjini kutodanganyika.

“Kwa niaba ya familia yangu na kwa niaba ya chama changu (CHADEMA), tunampa pole sana Mwakalebela kwa kuonewa na NEC ya CCM lakini tunawaomba wananchi wa Iringa, mfuteni machozi ndugu yetu huyu (Mwakalebela) kwa kuinyima kura CCM,” alisema Mchungaji Msigwa.

Mchungaji Msigwa ambaye uchaguzi wa mwaka 2005 aligombea jimbo hilo kupitia chama cha Tanzania Labour (TLP) alisema endapo atachaguliwa atawatumikia wananchi wa Manispaa ya Iringa kwa unyenyekevu mkubwa kwa sababu wao ndiyo waajiri wake.

Alisema atatumia vitivo mbalimbali vya Vyuo Vikuu vilivyopo Manispaa ya Iringa kuviunganisha na wananchi katika harakati ya kuvitumia Vyuo hivyo kuleta maendeleo.

Wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni pamoja na aliyekuwa kada wa CCM ambaye ametimkia CHADEMA na anagombea Jimbo la Njombe Kaskazini,Alatanga Nyagawa.

Nyagawa alijinasibu kuwa yeye, msigwa pamoja na aliyekuwa kada mwingine wa CCM aliyetimkia Chadema,Thomas Nyimbo tayari ni wabunge kutokana na kile alichokieleza kuwa wapinzania wao ni dhaifu.

“Tutatumia udhaifu wa wagombea wenzetu kushinda kwa kishindo,” alisema.

Moja ya udhaifu wa mgombea wa CCM katika jimbo la Njombe Kaskazini ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa Iringa,Deo Sanga maarufu Jah People,ni kudaiwa kuwa na elimu ya darasa la pili.

“Nitawaomba wananchi wa Njombe Kaskazini wamnyime kura Deo Sanga ili arudi MEMKWA (mpango maalum wa elimu kwa walioikosa),” alisema.

Hata hivyo,Sanga mwenyewe alipoongea na BLOG HII kwa simu alikanusha madai kwamba elimu yake ni darasa la pili bali akasema elimu yake ni darasa la saba na kwamba alisoma katika shule ya msingi Ikwega iliyopo wilayani Mufindi, ingawa alisema hakumbuki alihitimu mwaka gani.

“Mpaka nirejee kwenye kumbukumbu zangu ndiyo naweza kukueleza nilianza mwaka gani na nikamaliza mwaka gani,” alisema Deo Sanga, hata hivyo alipotafutwa baadaye alikuwa hapatikani.

Hata hivyo, alisema Nyagawa anayedai kwamba yeye (Sanga) ni mbumbumbu ni mfa maji anayetapatapa baada ya kuangushwa katika kura za maoni za CCM na kukumbilia CHADEMA.

No comments:

Post a Comment