Sunday, August 15, 2010

MCHUNGAJI MKWARE AFUTWA KAZI NA DAYOSISI

Na Mawazo Malembeka,Iringa

Agosti 15:KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, limemfuta kazi mwalimu na Mchungaji Michael Ngilangwa (35) anayekabiliwa na kesi mahakamani ya kuomba rushwa ya ngono na kutaka kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14 wa kidato cha kwanza wa shule ya sekondari ya Pomerin inayomilikiwa na Kanisa hilo.

Ngilagwa ambaye ni mwalimu wa kingiireza na masomo ya dini katika shule hiyo, alikamatwa Agosti 11, mwaka huu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Iringa akiwa nyumba ya kulala wageni iitwayo Wihanzi akiwa na mwanafunzi huyo.

Agosti 13, mwaka huu, Ngalingwa, alipandishwa kizimbani katika mahakama ya Mkoa wa Iringa na kusomewa mashitaka mawili ya kuomba rushwa ya ngono kwa binti mwenye umri wa miaka 14 kinyume cha sheria ya Kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 na kutaka kubaka kinyume na sheria ya jinai namba 16 ya mwaka 2002.

Akizungumza na Nipashe, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Iringa (DIRA), Nayman Chavalla alisema ofisi yake imemfuta kazi mwalimu huyo tangu Agosti 13,mwaka huu.

Alisema wamemfuta kazi kutokana na kufanya kitendo ambacho hakiungwi mkono na Kanisa, Dayosisi na wala shule ya Sekondari ya Pomerin.

“Kile kitendo tu cha kukutwa na mwanafunzi wake nyumba ya kulala wageni, tena usiku, kinatosha kutufanya sisi (DIRA) tuchukue maamuzi ambayo tumeona yanafaa, nayo ni kumfuta kazi mara moja,” alisema Chavalla.

Hata hivyo Chavalla alisema kuwa Ngilangwa hakuajiliwa kama Mchungaji na kwamba kwenye orodha ya wachungajiwa wa DIRA hayumo bali yumo kwenye orodha ya walimu wa DIRA.

Alisema mwalimu huyo ana shahada ya dini (Theolojia) na ni mwanafunzi wa shahada ya ualimu katika Chuo Kikuu huria na kwamba pale Pomerin aliajiliwa kama mwalimu.

Aidha, alisema kuwa, suala la Ngilangwa kufanya kitendo hicho kichafu, ni jambo binafsi na kwamba halina uhusiano wa shule, Dayosisi wala Kanisa.

“Utaona tangu suala hili likiwa mikononi mwa Takukuru hadi mahakamani, hakuna mtumishi wa shule, Dayosisi wala Kanisa aliyekwenda huko kutoa msaada wa aina yoyote,” alisema Chavalla.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment