Thursday, August 12, 2010

MAKADA WA CCM ZAIDI CORTIN, MWALIMU ANASWA KWA RUSHWA YA NGONO

Na Mawazo Malembeka

Agosti 12:MTUHUMIWA mwingine wa rushwa katika kura za maoni katika jimbo la Iringa Mjini,ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa,Fadhili Ngajilo, leo amepandishwa kizimbani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Ngajilo (31), ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu John cha Mjini Dodoma, alifikishwa mahakama ya Mkoa wa Iringa na kusomewa shitaka moja la kutoa hongo kinyume na sheria namba 11 ya kupambana na kuzuia rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010.

Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Consolatha Singano, Mwanasheria wa Takukuru,Prisca Mpepo alidai kuwa Ngajilo anadai kutoa hongo hiyo Julai 20,mwaka huu katika kijiji cha Mgongo,Manispaa ya Iringa.

Mwanasheria huyo alidai kuwa Ngajilo anadaiwa kutoa hongo ya Sh.30,000 kwa Kaimu Katibu wa CCM tawi la Mgogo,Gwido Sanga ili naye azigawe kwa wajumbe 30 wa CCM waliokuwa wamekusanyika kwenye nyumba ya Damas Mbilinyi kusubiri wagombea waliokuwa wanapita eneo hilo kujinadi.

Alidai kuwa hongo hiyo ililenga kuwashawishi wajumbe hao wampigie kura Ngajilo wakati wa kupiga kura za maoni.

Mtuhumiwa huyo alikana shtaka dhidi yake na Mwanasheria wa Takukuru, Prisca, alidai mahakamani hapo kwamba upelelezi haujakamilika na kwamba dhamana iko wazi kwa mtuhumiwa kama angetimiza masharti ambayo yangewekwa na mahakama hiyo.

Akisoma masharti ya dhamana kwa mtuhumiwa, hakimu Singano alisema mtuhumiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni wakazi wa Mkoa wa Iringa ambao pia wawe watumishi wa Serikali au taasisi yoyote inayotambulika kisheria na kwamba kila mdhamini asaini dhamana ya Sh.milioni mbili.

Hata hivyo, Ngajilo aliyekuwa anaonekana kujiamini muda wote wakati shaurio lake likisomwa, alikuwa ameandaa wadhamini wawili lakini mmoja ambaye alidaiwa kuwa ni baba yake alikataliwa na mahakama hiyo kwa kuwa nyaraka zake zilithibitisha kwamba siyo mtumishi wa serikali.

Hakimu Singano aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 06,mwaka huu, litakapotajwa tena na Ngajilo aliwekwa mahabusu wakati akisubiri kukamilisha taratibu za dhamana ambapo hadi majira saa saba mchana, alikuwa bado hajakamilisha taratibu hizo.

Watuhumiwa wengine kufikishwa mahakamani jana ni pamoja aliyewahi kuwa waziri kwa nyakati tofautitofauti na Mbunge wa siku nyingi wa jimbo la Mufindi Kaskazini,Joseph Munga akikabiliwa na makosa 15 ya rushwa.

Mwingine ni Frederick Mwakalebela ambaye licha ya kutokuwepo mahakama kwa taarifa, kesi yake ilifikishwa mahakamani na kusogezwa mbele hadi Agosti17,mwaka huu.

Wakati huo huo, Takukuru inamshikilia Mwalimu wa shule ya sekondari ya Pomerin iliyoko wilayani Kilolo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa,Michael Ngalingwa (35) kwa tuhuma ya kuomba na kupewa rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi wake wa kidato cha kwanza.

Taarifa zilizothibitishwa na Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa,Gasto Mkono, mwalimu huyo anadaiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza ili amsadie kufaulu vyema somo la kiingereza pamoja na kumpa ahadi ya kumsaidia matumizi madogomadogo awapo shuleni hapo.

Kwa mujibu wa Mkono, Takukuru walipewa taarifa za tukio hilo na wasamalia wema na kuweka mtego ulifanikiwa kumnasa mwalimu huyo kwenye moja ya nyumba za kulala wageni Mjini Iringa, saa sita ya usiku wa kuamkia leo (Agosti 12) akiwa na binti huyo.

Mkuu wa shule hiyo ya Pomerin, Shadrack Nyaulingo hakupatikana kwa maelezo kuwa alikuwa njia kwenda Takukuru kutoa baadhi ya taarifa muhimu zinazohusiana na tukio hilo.

Hata hivyo,msemaji mmoja wa Ofisi ya Dayosisi ya Iringa, (DIRA), ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa maelezo kuwa ofisi hiyo haihusiki na sula hilo kwa kuwa ni la binafsi zaidi (la Mwalimu aliyekamatwa) alikiri kuwepo kwa tukio hilo.

“Hata sisi tumepata taarifa hizi, ni kweli lakini naomba mtafute Mkuu wa shule atakueleza vyema, sisi (DIRA) hatuhusiki nalo kwa sababu ni la binafsi sana,” alisema kwa upole.

Mwisho

No comments:

Post a Comment