McEddy Elroy

Wednesday, August 11, 2010

TAKUKURU IRINGA YAANZA KAZI,MUNGAI CORTINI

Agosti 11:TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo imeanza rasmi kuwapandisha kizimbani makada wa CCM waliotuhumiwa kutoa rushwa wakati wa kampeni za kura za maoni kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama hicho katika nafasi ya ubunge kwenye majimbo yao.

Waliokuwa wa mwanzo kuonja shubiri hiyo ya kupandishwa kizimbani ni pamoja na Mbunge wa Mufindi Kaskazini,Joseph Mungai na aliyeongoza kura za maoni jimbo la Iringa mjini,Frederick Mwakalebela.

Mungai (66), kwa pamoja na watu wengine wawili ambao ni pamoja na Katibu wa Umoja wa vijana wa CCM wa wilaya ya Mufindi,Fidel Cholela (39) na Moses Masasi wamefikishwa katika mahakama ya Mkoa wa Iringa wakikabiliwa na mashtaka 15 ya rushwa kinyume na sheria ya kuzuia na kupamna na rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010 .

Kwa upande wa Mwakalebela, shauri lake lenye tuhuma moja ya rushwa, limefikishwa katika mahakama hiyo ya Mkoa lakini limesongezwa mbele hadi Adosti 17,mwaka huu, kwa kuwa alikuwa na ruksa ya kutokuwepo mahakamani leo.

Mbele ya hakimu wa mahakama ya Mkoa wa Iringa,Merry Senapee, msoma mashtaka wa Takukuru,Prisca Mpepo alidai kuwa mnamo Julai 08,mwaka huu, katika kata ya Ihalimba, wilaya ya Mufindi, Mungai akiwa mmoja wa makada wa CCM waliokuwa wanawania kupitishwa katika kura za maoni kugombe ubunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini kwa pamoja na watuhumiwa wenzake, walitoa hongo ya Sh.10,000 kwa Mwenyekiti wa CCM tawi la Vikula kama kishawishi cha kumpigia kura wakati wa zoezi la kura za maoni.

Katika shtaka la pili, watuhumiwa wote kwa pamoja, siku na eneo hilo walitoa hongo ya Sh.10,000 kwa Konjesta Kiyeyeu ambaye alihudhuria kikao cha kamati ya CCM kijiji cha Vikula.

Msoma mashtaka aliendelea kudaia mahakamani hapo kuwa, katika shtaka la tatu, nne, tano na sita, watuhumiwa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.10,000/- kwa kila mmoja kwa Aldo Lugusi, Ezekiel Mhewa, Tulaigwa Kisinda na Jiston Mhagama kwa lengo hilihilo la kuwashawishi wampigie kura za maoni.

Shtaka la saba wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.20,000 kwa Maria Kihongosi na shtaka la nane kutoa hongo ya Sh.5,000 Lurent Mdalingwa wakati shtaka la tisa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.20,000 kwa Victory Kalinga ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kijiji cha Ugessa.

Katika mashtaka namba kumi hadi 12 washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa walitoa hongo ya Sh.2,000 kwa kila mmoja kwa Francis Chonya, Alfred Kisinga na Issac Tewele wakati shtaka la 13 wanadaiwa walitoa hongo ya Sh.10,000 kwa Sosten Kigahe.

Aidha, msoma mashtaka huyo alidai kuwa shitakana namba 14 watuhumiwa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.10,000 kwa Raphael Lutumo na shitaka la mwisho walitoa hongo ya Sh.20,000 kwa Andrew Mkiwa.

Watuhumiwa wote walikana mashtaka na hakimu Senapee alisema dhamana iko wazi kwa watuhumiwa kwa masharti kwamba kila mtuhumiwa awe na wadhamini wawili ambapo mmoja wa wadhamini hao awe anaishi Manispaa ya Iringa na kila mdhamini asaini bondi ya Sh.milioni tano.

Hadi wandishi wa habari hii wanatoka mahakamani majira ya saa tano asubuhi, si Mungai wala watuhumiwa wengine waliokuwa wametimiza masharti ya dhamana hivyo waliswekwa mahabusu ya mahakama wakisubiri jamaa zao kutimiza masharti ya dhamana.

Taarifa zilizopatikana baadaye majira ya saa 8.30 alasiri kutoka mahakamani hapo zilithibitisha kuwa watuhumiwa wote walitimiza masharti ya dhamana na kwamba shauri hilo litarejeshwa mahakamani hapo kwa kutajwa Agosti 25,mwaka huu.

Kwa upande wa shitaka lililofikishwa mahakamani hapo likimkabili Mwakalebela, lilidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa la rushwa Juni, mwaka huu, katika kijiji cha Mkoga,Manispaa ya Iringa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ya Takukuru,Mwakalebela anadaiwa kutoa hongo ya Sh.100,000 kwa Mwenyekiti wa CCM wa kijiji hicho,Hamisi Luhanga ili naye azigawe kwa wapiga kura wa CCM ambao wangempigia kura wakati wa zoezi la kura za maoni.

Mwakalebela alikuwa na udhuru hivyo shauri lake lilisongezwa mbele hadi Agosti 17,mwaka huu.

Hata hivyo, Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Iringa,Bonasian Kessy alisema Mwakalebela anashitakiwa kwa makosa mawili ya rushwa na kwamba shtaka lingine litafikishwa mahakamani kesho (Agosti 12) ingawa hakutaka kulifafanua.

Kamanda Kessy pia alithibitisha kuwa mtuhumiwa mwingine wa rushwa katika kampeni za kura za maoni ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa CCM Mkoa wa Iringa,Fadhili Ngajilo pia atapandishwa kizimbani kesho (Agosti 12) kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment