CHAMA cha Tanzania Labour (TLP) Mkoa wa Iringa, kimepata pigo baada ya ofisi yake kufungwa na samani zote za ofisi hiyo kushikiliwa kwa ajili ya kupigwa mnada na kampuni ya udalali ya Majembe.
TLP iliyokuwa imeweka Ofisi zake katika jengo la Akiba House linalomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) hadi sasa haina Ofisi na hivyo kuwafanya viongozi wake kuhaha mitaani.
Ofisi hiyo ilivunjwa juzi na vifaa vyote kuchukuliwa na Kampuniya Majembe ikiwemo mafaili na nyaraka mbalimbali kutoka na Chama hicho kudaiwa pango la zaidi ya Shilingi 2,400,000.
Jana mchana Nipashe iliwashuhudia watumishi wa kampuni ya udalali ya majembe wakiondoa samani za ofisi hiyo na kuzipakia kwenye magari yao na kisha kuifunga ofisi hiyo kwa makufuli maalumu.
Katibu wa TLP Mkoa wa Iringa, Mrisho Samson na Katibu Mwenezi wa Mkoa huo Francis Blanka walifika baadaye ofisini hapo na kujaribu kuoko baadhi ya nyaraka lakini walikataliwa na wafanyakazi hao wa Majembe.
Meneja wa Operesheni wa Majembe, Mussa Moto hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba jambo hilo waulizwe NSSF ndiyo waliowapa kazi hiyo ya kuwatoa baadhi ya wapangaji.
Kwa upande wake,Meneja wa NSSF Mkoa wa Iringa, Bathow Mmuni, alisema hawakuwa na lengo lolote la kisiasa dhidi ya TLP bali wako kwenye operesheni ya kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa sugu.
Alisema TLP ni mmoja wa wapangaji ambao ni wadaiwa sugu katika jengo hilo la ‘Akiba House’ na kwamba hawakuwa na njia mbadala bali ni kuwaondoa kwenye jengo kutokana na kushindwa kulipa kodi kwa zaidi ya miaka miwili.
Alisema katika operesheni hiyo,jumla ya wapangaji 33 waliopo kwenye majengo mbalimbali ya vitega uchumi vya NSSF Mkoani Iringa, walikuwa ni wadaiwa sugu ambapo baada ya shughuli hiyo ya kukusanya madeni kukabidhiwa kwa Majembe Auction Mart,zaidi ya Sh.milioni 54.5 zimekusanya.
Alisema wapamgaji tisa wakiwemo TLP ambao wameshindwa kulipa madeni, wameondolewa kwa nguvu na mali zao hususani samani za ofisi zimetaifishwa mpaka watakapolipa madeni na wakishindwa samani hizo zitauzwa kwa mnada.
Katibu wa Mkoa wa TLP,Samson hakutaka kulizungumzia suala hilo kwa maelezo kuwa siyo msemaji lakini Katibu Mwenezi,Blanka alikiri TLP kudaiwa Sh.2,400,000 ikiwa ni kodi ya pango.
Hata hivyo, alisema Chama chake (TLP) Taifa kimeshakiri kulitambua deni hilo na walikuwa wameandika barua kwa NSSF kwamba watachelewa kidogo kulipa kwa sababu Mwenyekiti wa Taifa,Agustino Mrema ambaye alipaswa kusaini hundi ya malipo hayupo Dar-es-Salaam.
Mrema Mwenyewe alipopigiwa Simu alijibu kwa kifupi tu kisha kukata simu: “Mimi nahangaikia Jimbo langu la Vunjo bwana hayo mambo ya ofisi siyajuwi”.
TLP ni moja ya vyama vya upinzani vilivyosimamisha wagombea wa ubunge katika Jimbo la Kalenga na katika majimbo mengine kimekuwa pega kwa pega kuwaunga mkono wagombea wengine wa vyama vya upizani na sasa kimetaifishwa ofisi ya kuratibu shughuli hizo za kampeni.
No comments:
Post a Comment