McEddy Elroy

Tuesday, August 17, 2010

MASHITAKA DHIDI YA MWAKALEBELA

HATIMAYE Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Frederick Mwakalebela (41) na mkewe Selina Mwakalebela, wanaokabiliwa na tuhuma ya rushwa katika mchakato wa kura za maoni za kumpata mgombea ubunge wa chama hicho Jimbo la Iringa Mjini, wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Awali,Mwakalebela alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilayani Iringa, kwa ajili ya kusomewa shitaka la kwanza ambalo ni kesi ya Jinai namba 4 ya mwaka 2010, inayohusiana na kutoa hongo kinyume cha sheria namba 15 (1) (b) ya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo ilisomwa pamoja na kifungu cha cha 21 (1) ( a) na 24 (8) ya Sheria ya gharama za Uchaguzi.
Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Festo Lwila wa Mahakama ya Hakimu mkazi Wilaya ya Iringa.
Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Imani Nitume aliyekuwa akisaidiwa na Prisca Mpeka alidai kuwa Mwakalebela alitenda kosa hilo mwezi Juni mwaka huu katika kijiji cha Mkoga katika Manispaa ya Iringa.

Mwakalebela anadaiwa kutoa hongo ya Sh.100,000 kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamisi Luhanga ili azigawe kwa wapiga kura 30 wa CCM ili wampigie kura za maoni za kumchagua mtuhumiwa wa kwanza (Mwakalebela), 01/08/2010 .

Mtuhumiwa huyo alikana kosa hilo na Hakimu Lwila alisema dhamana iko wazi kwa Mwakalebela ambapo alitoa masharti ya dhamana hiyo ambayo ni pamoja na ahadi ya shilingi milioni 5000,000 kwa kila mdhamini.

Mwakalebela alidhaminiwa na wadhamini wawili ambao mmoja wao ni mtumishi wa Serikali. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 15 mwaka huu itakapotajwa tena.

Katika kesi ya pili namba 8, ya mwaka 2010,inayomkabili pia mtuhumiwa Frederick Mwakalebela na Mkewe Selina Mwakalebela, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru Imani Nitume alidai mbele ya mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kutoa hongo ya shilingi 100,000 kinyume na vifungu vilivyotajwa hapo juu.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu mkazi Mkoa wa Iringa, Gladys Barthy.

Hata hivyo,wakati kesi hiyo ikiendelea, yalijitokeza mabishano ya kisheria kati ya Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Imani Nitume na Wakili wa Kujitegemea Basil Mkwata anayemtetea Mwakalebela na mkewe Selina, kutokana na mahakama kutaka kujiridhisha na nyaraka zilizotumiwa na baadhi ya wadhamini.

Baadhi ya nyaraka za wadhamini (barua) waliojitokeza mahakamani hapo zilikuwa hazijakamilika na Mwendesha mashitaka wa Takukuru na Wakili huyo walikuwa wakibishana kuhusiana na utata huo, ingawa baadae walipatatikana wadhamini waliokuwa na nyaraka timilifu.

Watuhumiwa wote wawili wamekana kosa hilo na wameachiwa kwa dhamana hadi hapo kesi hiyo itakapotajwa tena Septemba 15 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment