Friday, August 13, 2010

MHASIBU WAKALA WA MAJENZI CORKOTINI

Na Mawazo Malembeka,Iringa

Agosti 13: MHASIBU Msaidizi wa Wakala wa Majenzi (TBA) Mkoa wa Iringa,Benjamin Mbope (56),amepandishwa kizimbani kwa makosa 94 ya kula njama, kughushi na kuibia wakala hao zaidi ya Sh.35.3

Mhasibu huyo msaidizi amefikishwa mahakamani jana (Agosti 12) katika mahakama ya wilaya ya Iringa.

Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo,Festo Lwila,Mwendesha mashitaka,Mrakibu msaidizi wa polisi,Matiku, alidai kuwa, kati ya Disemba 2, mwaka jana na Juni 8,mwaka huu, mtuhumiwa alitenda makosa hayo.

Matiku alidai kuwa, Desemba 2 mwaka jana, kwa nia ya kuidhulumu wakala hiyo, mtuhumiwa alikula njama na watu wasiojulikana na kuiba jumla ya Sh.35,377,300.

Aidha, Matiku aliendelea kuieleza mahakama hiyo kwamba, Desemba 23, mwaka jana, mtuhumiwa alighushi saini ya Meneja wa Wakala hiyo, Bartazar Kimangano na kuiba Sh.1,780,300 huku akijua kuwa ni kosa la jinai.

Mahakama hiyo iliendelea kuelezwa kwamba, Mhasibu huyo msaidizi aliandaa na hatimaye kuandika cheki yenye namba 3896729 na kuiba kiasi hicho cha fedha kutoka kwenye akaunti ya wakala hiyo yenye namba 01J1027842011 iliyopo benki ya CRDB Mkoa wa Iringa.

Katika kosa la kumi hadi 94, ilielezwa mahakamani hapo kwamba kati ya Disemba mwaka jana na Juni mwaka huu, mtuhumiwa huyo kwa nyakati tofauti alikuwa akiandaa hati za malipo na kuandika cheki na kuiba viwango tofauti tofauti cha fedha kinachofikia zaidi ya Sh.milioni 35.3.

Upande wa mashitaka ulisema dhamana kwa mtuhumiwa iko wazi ikiwa mtuhumiwa angetimiza masharti yatakayowekwa na mahakama.

Akisoma masharti ya dhamana, hakimu Lwila alisema mtuhumiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja amdhamini mtuhumiwa kwa Sh.milioni 40 na kwamba mmoja wa wadhamini hao lazima awe na mali isiyohamishika katika Manispaa ya Iringa, yenye thamani ya Sh.milioni 30.

Mtuhumiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na alipelekwa gereza la mahabusu hadi Agosti 26,shauri hilo litakapolejeshwa mahakamani hapo kwa kutajwa.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment