McEddy Elroy

Monday, August 30, 2010

WAODAI STAKABADHI KUBANWA NA SHERIA

Agosti 30:MAMLAKA ya Mapato (TRA) Mkoa wa Iringa imewatahadharisha wananchi kuwa watakumbana na mkono wa sheria ikiwa wataendelea kununua bidhaa mbalimbali bila kudai sitakabadhi ya manunuzi yao.

Akizungumza na blog hii ofisini kwake,Menaja wa TRA Mkoa wa Iringa,Rosalia Mwenda alisema sheria iliyowezesha kuwepo kwa mashine maalumu za kielektroniki (EFD) za kutoa stakabadhi na kutunza kumbukumbu, inambana pia mnunuzi kudai risiti kwa kila bidhaa anayouziwa.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, sheria hiyo inawataka wafanyabiashara wote walioandikishwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kufunga mashine hizo kwenye maeneo yao ya biashara.

“Moja ya vikwazo vya kukusanya kodi ambavyo vimetukabili muda mrefu ni wananchi kutokuwa na utamaduni wa kudai syakabadhi, kwa bahati nzuri sheria ya mashine hizi za EFD inambana pia mtu ambaye atakuwa na bidhaa lakini akiwa hana stakabadhi, hivyo tunaomba wananchi kila wanaponunua bidhaa wadai stakabadhi vinginevyo watashitakiwa mahakamani” alisema.

Alisema EFD (Electronic Fiscal Device) ni mashine ambayo hutoa stakabadhi na kutunza kumbukumbu za kibiashara kwa muda wa miaka mitano na pia zitakuwa zinatoa taarifa TRA juu shughuli zote za kibiashara zinazofanywa na mfanyabiashara mwenye mashine hiyo kwa njia ya kielektroniki.

Alisema mwaka huu wa fedha yaani kuanzia Julai, 2010 hadi Juni 2011 TRA Mkoa wa Iringa imepangiwa kukusanya zaidi ya Sh.bilioni 23.112 ikiwa ni ongezeko la asilimia 32 ikilinganishwa na lengo la mwaka wa fedha wa 2009/2010.

Alisema mwaka wa fedha wa 2009/2010 walipangiwa kukusanya Sh.bilioni 16.773 lakini wakavuka lengo kwa kukusanya Sh.bilioni 17.663 sawa na asilimia 105 ya lengo.

Mwenda alisema waliweza kuvuka lengo kutokana na mikakati waliyojiwekea na kuitekeleza vyema ikiwa ni pamoja na kuweza kutekeleza shughuli ya ukaguaji wa hesabu za walipakodi hali iliyowaongezea makusanyo ya kodi.

Mkakati mwingine ni ukusanyaji kodi kwa vitalu, yaani maafisa wa TRA wamekuwa na utaratibu wa kuangalia hali halisi ya baishara za wafanyabiashara ikilinganishwa na nyuma ambapo wafanyabiashara wenyewe ndiyo walikuwa wanatamka kiwango cha mtaji walichonacho na kukadiriwa kodi.

Alisema elimu kwa mlipakodi imewasaidia pamoja na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi imekuwa ni chachu hiyo ya kuvuka lengo.

No comments:

Post a Comment