McEddy Elroy

Tuesday, August 31, 2010

CHUO KIKUU MKWAWA WATEMBEZA BAKULI KUOMBA MSAADA

Agosti 31:CHUO Kikuu kishiriki cha Elimu cha Mkwawa cha Mkoani Iringa (MUCE),kimeyalilia mashirika na wahisani mbalimbali kuliokoa jahazi la Chuo hicho ambalo limeelezwa kuwa linazama kila kukicha.

Akizungmza na ugeni wa Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF),uliotembelea Chuoni hapo leo (Agosti 31) Mwanasheria Mwandamizi wa Chuo hicho,Alfred Nyamwangi amesema Chuo hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi zinazowafanya ustawi wa Chuo hicho uwe wa kusuasua.

Ugeni huo pamoja na mambo mengine, ulifika Chuo hapo kuchangia mfuko wa zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vyema katika masomo yao zawadi ambazo hutolewa katika mahafali ya Chuo hicho.

Moja ya Changamoto hizo alisema na kushindwa kuwa na miundombinu ya kuwalaza wanafunzi wote Chuoni hapo na hivyo kuwafanya wanafunzi wengi kuishi maeneo ya hatari.

Alisema miundombinu inayotumika ni ile iliyokuwa inatumika wakati ikiwa ni Shule ya sekondari ya Mkwawa.

Alisema mabweni waliyonayo, kwa mfano, yana uwezo wa kulaza wanafunzi 1060 ikiwa ni chini ya asilimia 60 ya wanafunzi wote. Chuo hicho kwa sasa kina zaidi ya wanafunzi 1,900.

Aidha, alisema hakuna jengo la utawala na kwamba wahadhiri wamekuwa wakitumia ofisi zilizokuwa za walimu wa sekondari.

“Kimsingi hatuna ofisi hata moja vivyo hivyo jengo la Utawala na hali hii imekuwa inatishia ustawi wa Chuo chetu,” alisema Nyamwangi.
Alisema Chuo hicho kinahitaji kumbi nne za mihadhara na kwamba moja ndiyo kwanza imeanza kujengwa kwa fedha za serikali na nyingine inaweza kuanza kujengwa mwakani kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Kufuatia Changumoto hizo,Nyamwangi aliiomba LAPF kutumia mfumo wa Jengo, Tumia na Hamisha ambapo inaweza kuingia mkataba na Chuo hicho, ikapewa eneo la kujenga na baada ya miaka kadhaa majengo hayo yakamilikishwa kwa Chuo hicho.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi hundi ya Sh.laki tatu kwa uongozi wa MUCE,Meneja Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano wa LAPF,Andrew Kuyeyana alisema licha ya kitoa kiasi hicho kidogo cha fedha kwenye mfuko wa kuwamotisha wanafunzi wa Chuo hicho, LAPF itaendelea kuchangia kwenye mfuko huo kila mwaka.

Aliuomba uongozi wa MUCE wakutane na uongozi wa LAPF ili kuona ni namna gani nzuri ya kusaidiana kutatua changamoto zinazokikabili Chuo hicho.

Aidha,Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho, anayeshughulikia Utawala,Professa John Machiwa aliishukuru LAPF kwa kutambua umuhimu wa kuwamotisha wanafunzi lakini pia kuonyesha nia ya kuchangia katika kutatua changamoto za Chuo hicho.

No comments:

Post a Comment