Wednesday, September 1, 2010

WAPINZANI IRINGA WAWEKA KANDO KAMPENI,WAANZA VITA YA MATUSI

Septemba 01:BAADHI ya wakazi wa Jimbo la Iringa mjini wamelaani vikali vitengo vya baadhi ya wafuasi wa wagombea wa ubunge wa jimbo hilo kuanza kampeni chafu za kurushiana matusi majukwaani.

Wananchi hao pia wametoa masikitiko na kuonyesha wasiwasi kama wafuasi hao wana nia njema na Jimbo hilo kutokana na kuacha kazi ya kueleza mikakati ya namna gani nzuri watakavyowahudumia wananchi na kutumia muda mrefu kutukanana.

Aidha, wananchi hao wamefikia hatua ya kuwalaani baada ya wafuasi wa Mgombea wa Ubunge Jimbo la Iringa Mjini kupitia unaojiita ‘Muungano wa Upinzani’, Mariam Mwakingwe kupanda jukwaani na kuanza kurusha matusi katika mkutano wa kampeni,Jumanne, Agosti 31,mwaka huu katika Stendi ya Mkoa wa Iringa.

Francis Blanka ambaye ni Katibu Mwenezi wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Mkoa wa Iringa na Benny Kapwani ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chma cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Iringa, kwa nyakati tofauti jana walipanda jukwaani na kuvurumisha matusi yasiyoandikika.

Walikuwa wanamshambulia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA,Chiku Abwao, ambaye katika uzinduzi rasmi wa kampeni za CHADEMA Mkoa wa Iringa, alidai kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wao (CHADEMA) Mkoa wa Iringa alijiuzulu wadhifa huo baada ya chake chake kubaini kuwa amenunuliwa na CCM ili kuwahujumu.

Mwingine aliyekuwa akiporomoshewa matusi hayo ni mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kupitia CHADEMA,Mchungaji Peter Msigwa
Chiku alidai kuwa,wanazo taarifa kwamba Kapwani ambaye alikuwa amechukua fomu za kuwania ubunge Jimbo la Isimani hakurejesha fomu hizo kutokana na kununuliwa na mgombea mwingine ambaye amekuwa Mbunge wa Isimani kwa miaka 15 na ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam,William Lukuvi,hivyo mgombea huyo wa CCM kupita bila kupingwa.

Ndipo vurugu zilipoanza ambapo jana Kapwani na Blanka walishirikiana kurusha matusi hayo kwa Abwao na Msigwa na kufanya baadhi ya watu waamini kuwa huenda watu hao walikuwa ‘wamechanganyikiwa’.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walisema wamesikitishwa na hali hiyo na kuitaka Serikali kupitia ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwaonya watu hao kama si kuwafuta kabisa kwenye kampeni.

“Tulikuja kusikia sera zao lakini kama tungejua kwamba tunakuja kusikia watu na heshima zao wakitukana hadharani wala tusingepoteza muda wetu,” alisema mkazi wa Ilala iliyetambulisha kwa jina la Elisha Mhanga.

Chiku Abwao mwenyewe aliiambia Blog hii baadaye kuwa alikuwa anakusanya ushahidi ili awasilishe kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Iringa Mjini kabla ya kufungua kesi mahakamani kwa sababu wazungumzaji walimshambulia yeye binafsi na biashara zake.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo,Theresia Mahongo alisema hakuwa amepata malalamiko yoyote lakini akavikumbusha vyama vya siasa kuzingatia maadili ya Uchaguzi waliyosaini vinginevyo watashughulikiwa.

“Binafsi sikuyasikia hayo matusi kwa sababu sikuwepo kwenye mkutano wao lakini nitafuatilia ili niwakumbushe kwamba kampeni siyo njia ya kuchochea uvunjifu wa mshikamano na amani tuliyonayo,” alisema Mahongo.

Umeibuka mpasuko mkubwa katika kambi ya upinzani Mjini Iringa mpasuko ambao ni dhahiri unaweza kumnufaisha mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kupitia CCM,Monica Mbega ambaye naye ana wakati mgumu kutokana na mpasuko ndani ya CCM katika Jimbo hilo unaodaiwa kuwepo baada ya aliyeongoza katika kura za maoni,Frederick Mwakalebela, kuenguliwa na NEC ya CCM.

Katika kambi ya upinzani,vyama vya TLP,CUF,APPT na NCCR-Mageuzi vinamuunga mkono mgombea kupitia NCCR-Mageuzi,Mariam Mwakingwe huku CHADEMA wakiwa hawautambui muungano huo hali ambayo imeleta uhasama mkubwa na kuanza kushambulia peupe kwenye majukwaa ya kampeni.

Mwisho

No comments:

Post a Comment