McEddy Elroy

Wednesday, September 8, 2010

NCCR-MAGEUZI IRINGA KIKAAONGONI

MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Iringa Mjini,Theresia Mahongo amekitaka Chama cha NCCR-Mageuzi kuitisha mkutano wa hadhara kuwaomba radhi mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kupitia Chadema,Mchungaji Peter Msigwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,Chiku Abwao.

NCCR-Mageuzi pia imetakiwa kuandika barua ya kuwaomba radhi Mchugaji Msigwa na Abwao na nakala yake kutumwa kwa Msimamizi huyo wa Uchaguzi Jimbo la Iringa Mjini.

Agizo hilo la Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Iringa kwa Chama cha NCCR-mageuzi limekuja siku tano baada ya wafuasi wa Mgombea wa Ubunge jimbo hilo kupitia Chama hicho cha NCCR-Mageuzi,Mariam Mwakingwe, kupanda jukwaani na kurusha matusi yasiyoandika katika mkutano wa kampeni uliofanyika Stendi ya Mabasi,Mjini Iringa,Agosti 31,mwaka huu.

Wafuasi hao ni Francis Blanka ambaye ni Katibu Mwenezi wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Mkoa wa Iringa na Benny Kapwani ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Iringa, kwa nyakati tofauti katika mkutano huo wa kampeni walipanda jukwaani na kuvurumisha matusi yasiyoandikika kwa mchungaji Msigwa na Abwao.

Kwa mujibu wa barua ya Mahongo ya Septemba 06,mwaka huu, kwenda kwa NCCR-Mageuzi ambayo Nipashe imepata nakala yake, Msimamizi huyo pia amekiagiza Chama hicho kuacha kumpeni za matusi vinginevyo kitatozwa faini ya Sh.100,000 au kufutwa kwenye kampeni hadi Oktoba 31,mwaka huu.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 5:8 (a) cha maadili ya Uchaguzi, (NCCR) mnaagizwa kuomba radhi hadharani katika eneo lilelile mlilotumia kutoa lugha ya kashfa. Mnaagizwa kutuletea tarehe utakayofanya mkutano huo wa kuomba radhi ndani ya siku tatu ili Kamati ya Maadili ya Uchaguzi uhudhurie kwa ajili ya kujiridhisha,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Maagizo hayo kwa NCCR-Mageuzi yaliyotolewa na Msimamizi huyo wa Uchaguzi,yanafuatia kikao cha Maadili ya Uchaguzi kilichoketi Septemaba 04,mwaka huu kujadili malalamiko yaliyowasilishwa kwenye kamati hiyo na Mchugaji Msigwa pamoja na Abwao.

Barua ya malalamiko hayo iliyosainiwa na Katibu wa Chadema Iringa Mjini,Suzane Mgonakulima, iliitaka ofisi ya Msimamizi huyo kuchukua hatua mara moja kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa ili kuepusha uvunjifu wa amani katika Jimbo hilo.

Katibu wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Iringa,James Mwamgiga amekiri kupokea barua ya msimamizi huyo lakini amesema hawataitekeleza na badala yake wamekata rufaa.

“Barua ile imekuja tofauti na tulivyokubalina kwenye kikao cha maadili, kuna maneno yameongezwa ikiwemo kuwaandikia (Mchungaji Msigwa na Abwao) barua ya kuwaomba radhi,..tunasubiri kwanza maamuzi ya rufani yetu,” alisema Mwamgiga.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment