Saturday, October 1, 2011

UMWAGILIAJI SAWA,UMEME NAO JE?????????????

Ukichunguza kwa makini,utabaini kwamba uchache wa mvua katika misimu miwili iliyopita siyo chanzo pekee cha kukauka kwa mto Ruaha Mkuu na hatimaye kukauka kwa bwawa la Mtera na mabwawa mengine kama Kidatu na Kihansi.

Kilimo cha umwagiliaji kinachopigiwa upatu mkubwa sana na tamko la Kilimo kwanza, ambacho hufanyika katika maeneo mbalimbali hususani maeneo ya Kapunga huko Mbarali, karibu kabisa na chanzo cha mto Ruaha Mkuu huko katika eneo oevu la Ihefu,kimekuwa ni chanzo kikubwa cha kukauka mto huo.

Kingine ni siasa chafu za baadhi ya wanasiasa wanajali zaidi maslahi yao na kuacha maslahi ya Taifa.Mathalani, Serikali ilikwishatangaza hadi kwenye gazeti la Serikali kwamba eneo flani liihifadhiwe na watu wote waliokuwepo waondoke ili uoto wa asili urejee na hivyo kutiririsha maji mwaka mzima lakini anaibuka mtu mmoja tu tena anayetaka ubunge na kuanza kuwalaghai wananchi kwamba Serikali ilifanya makosa na hivyo wakimchagua yeye atahakikisha wanarejea kwenye eneo hilo,ni nini hiyo kama siyo siasa chafu isiyozingatia maslahi ya Taifa na kwa hakika siasa kama hiyo inaweza kulitumbukiza Taifa katika vurugu na wananchi wake.

Ukiungalia mto Ruaha Mkuu kwa sasa, hauna matumaini kabisa kwa Taifa hili kwa upande wa umeme.Lakini mto huo unaonesha matumaini kidogo kadri unavyoelekea kwenye chanzo chake huko Ihefu.Kumbuka Ihefu ni matokeo ya maamuzi magumu yaliyofanywa na Serikali takribani miaka mitano iliyopita kwa kuwaondoa wafugaji waliokuwa wamevamia eneo hilo.

Kwenye hifadhi ya Ruaha,mto huo umebaki kuwa na hali ya madimbwi madogo madogo ambayo kwa sasa ndiyo uanaokoa wanyama waliomo humo lakini ukiufuatilia hadi Ihefu, utagundua kuwa,kadri unavyoelekea Ihefu, ndivyo unavyokuwa na uhai kidogo kama picha hapo juu, inavyoonesha.

No comments:

Post a Comment