Tuesday, December 7, 2010

MAWAZO YA MLIPUAJI WA KUJITOA MHANGA

Mambomu ya kujitoa mhanga yamekuwa mtindo wa mashambulio ya kisiasa katika zama zetu hizi. Kuanzia Afghanistan hadi Madrid, London mpaka Sri Lanka, mabomu hayo yamekuwa katika maisha ya kila siku ya kisiasa na ni mbinu muhimu inayotumiwa katika ugaidi wa kisasa.

Wakati uchunguzi wa milipuko ya Julai 7 jijini London ukiendelea kufanyika na kujaribu kuona kipi kilijiri siku hiyo, utafiti mdogo sana umefanyika kutazama nini hasa wanawaza walipuaji wenyewe wa kujitoa mhanga.

Sababu

Kujaribu kugundua hasa kwa nini mlipuaji wa kujitoa mhanga, anajiua ili kuendeleza harakati fulani, ni vigumu mno, na ni kwa sababu ambazo zinazoeleweka kabisa.

Lakini utafiti mmoja uliofanywa na Chuo Kikuu cha Tel Aviv, nchini Israel, umefanya bidii kujaribu kugundua iwapo walipuaji wa kujitoa mhanga wana tabia zozote zinazoonekana. Wamefanya hivyo kwa kuzungumza na kufanya tathmini ya watu waliokuwa wawe walipuaji wa kujitoa mhanga.

Watu hao, ambao walijaribu kufanya mashambulio ya kujitoa mhanga, lakini walishindwa kwa sababu mbalimbali, ikiwemo matatizo ya kiufundo (bomu halikulipuka) au kukamatwa kabla ya kujilipua (wakielekea kujilipua au mapema kabla ya hapo).

Msongo wa mawazo

Watafiti waligundua mkondo wa watu ambao hawana uwezo mkubwa wa kuhimili wanapojikuta katika hali ya msongo, au mfadhaiko utokanao na shida (stress). Aidha pia waligundua kuwa watu hao hawana uwezo wa 'kuona mbali' na pia kuwa na tabia ya kutishwa na watu wenye madaraka.

Vilevile wamegundua kuwa, watu wanaowaandaa walipuaji wa kujitoa mhanga, wana ubinafsi mkubwa, wana uwezo mkubwa wa kiakili kupambana na msongo, na mara nyingi, wenyewe hawako tayari kuwa walipuaji wa kujitoa mhanga.

Profesa mstaafu, na mtaalam wa masuala ya ugaidi Ariel Merari, aliweza kukutana na watu 15 waliokuwa wakitaka kujilipua, ambao wako gerezani, kwa tuhuma za mashambulio yanayohusiana na mzozo wa Israel na Palestina.

Watano kati yao, walikuwa wametumwa na kundi la Hamas, watano na kundi la Islamic Jihad na watano kutoka kundi la al-Aqsa la Fatah.

Waandaaji

Aidha, Profesa Merari na wataalam wenzake waliziungumza na waandaaji wa walipuaji hao, wote kutoka makundi hayo.

Mbali na waandaaji hao na walipuaji wa kujitoa mhanga, kulikuwa na kundi la udhibiti. Kundi hilo la watu 12 walikuwa wameshitakiwa na kufungwa kwa ghasia mbalimbali za kisiasa kuanzia urushaji mawe hadi mashambulizi ya kutumia silaha.

Changamoto ya kwanza kwa kikosi cha Profesa Merari ilikuwa kuwashawishi watu hao kuzungumza. Wafungwa hao walisisitiza kupata ruhusa kwanza kutoka kwa wakubwa wa makundi yao.

"Niliwaambia sababu za sisi kufanya utafiti huu," amesema Profesa Merari akizungumza na kituo cha BBC Radio 4.

"Kulikuwa na mjadala mzito. Mwishowe walikubali kushiriki na hakika hiyo ndio ilikuwa hatua muhimu kupata wengine kuweza kuzungumza."

Katika miaka ya hivi karibuni, ulipuaji wa kujitoa mhanga umeongezeka duniani.Kati ya mwaka 1981 na 2000, nchi 17 zimeathiriwa na mashambulio ya kujitoa mhanga, ikilinganishwa na nchi 32 kati ya mwaka 2001 na 2008.

Waumini

Mashambulio ya kujitoa mhanga mara nyingi huhusishwa na mtazamo wa itikadi kali za kidini kutoka kwa mshambuliaji.

Hata hivyo, utafiti huu mpya unasema, umuhimu wa dini haukupewa nafasi ya juu, ikilinganishwa na sababu nyingine, wakati wafungwa hao wakizungumzia wakati wakifanya uamuzi wa kuendesha mashambulio hayo ya kujilipua.

"Karibu wote walikuwa watu wanaofuata dini, lakini waliokuwa wakitaka kujilipua hawakuwa waumini sana kama wale wanaowadhibiti.

"Undani na ukubwa wa imani ya kidini haukuwa jambo ambalo liliwatofautisha kati yao na magaidi wasiotumia njia ya kujilipua."

Badala yake, Profesa Merari amegundua kuwa "Kuaibishwa kwa taifa" ndio sababu kuu ya kufanya mashambulio hayo.

"Hii ndio sababu kubwa, ya wazi na yenye nguvu iliyowapa ari ya kufanya hivyo.

"Sio suala la mtu kuteseka binafsi; walijaribu kulipiza kisasi kwa niaba ya jamii yao inayoteseka. wametaja matukio ambayo wameyaona katika televisheni, na sio matukio yaliyowatokea wao binafsi."

Watu waliohojiwa katika nafasi ya uandaaji wa walipuaji, walikuwa kwa wastani wakubwa kiumri, wenye elimu ya kutosha na ambao wasingependa wao kujitokeza na kujilipua.

Tisa kati ya 14 walikiri kuwa wasingekuwa tayari wao wenyewe kujilipua, kwa sababu- walikuwa wanaogopa kufanya hivyo

"Hawakutumia neno 'kuogopa', lakini walitumia maneno kama vile 'sio kila mtu anaweza kufanya hivyo', au 'inahitaji mtu mwenye hiba ya kipekee' na maneno kama hayo.

"watano waliosalia walisema 'kimsingi ningependa kufanya hivyo, lakini kazi yangu kama kamanda ni muhimu kwa hiyo sikuweza kufanya hivyo'. Walikuwa waoga tu nadhani, katika kutoa jibu la moja kwa moja."

Picha halisi

Utafiti huo pia uligundua kuwa taswira inayowekwa na waandaaji wa walipuaji wa kujitoa mhanga, kuwa "ni vijana wenye dhamira kubwa" ni jambo la kupotosha.

"Walipuaji wa kujitoa mhanga wenywe wametoa taswira tofauti kabisa. Asilimia sitini na sita walikiri kuwa walikuwa wakiogopa kufanya hivyo, au walikuwa wakisita. Na tulivyochunguza idadi kubwa ya matukio ya kujilipua, tuligundua asilimia 36 ya matukio 61 ya walipuaji wa kujitoa mhanga, waliamua kuacha kufanya hivyo.

Profesa Merari anakiri kuwa, kwa sababu watu wote waliozungumza nao wametokana na majaribio "yaliyoshindwa kufanikiwa", utafiti huu hauwezi kutoa picha halisi ya mlipuaji wa kujitoa mhanga.

Hata hivyo, timu hiyo ya wataalamu inaamini utafiti huo unatoa "picha ya karibu zaidi".

"Baadhi ya walipuaji hawa wa kujitoa mhanga walifika kabisa na katika maeneo waliyotakiwa kujilipua, na hata kubonyeza kitufe cha kujilipua, lakini mabomu waliyokuwa wameyabeba hayakulipuka, kutokana na sababu za kiufundi.

"Kisaikolojia, hawa ni walipuaji wa kujitoa mhanga kwa kila mtazamo."

Utafiti wake huu unafikia majumuisho kuwa, hatua zinaweza kuchukuliwa kuzuia mashambulizi kwa misingi ya kutazama haiba na tabia ya mtu.

"Moja ya majumuisho ya utafiti huu ni kuwa kizuizi chochote kitakapomkabili mlipuaji wa kujitoa mhanga, kunaongeza nafasi ya mlipuaji huyo kubadili mawazo yake kutekeleza shambulio. Hii ni kwa sababu, wale wanaosita huhitaji kisingizio cha kutofanya shambulio.

"Wanahitaji kisingizio ili wasipoteze heshima yao binafsi.

"Kikwazo chochote, kitakwimu, kitaongeza nafasi ya mlipuaji wa kujitoa mhanga kubadili mawazo yake, akiwa njiani kwenda kujilipua."

No comments:

Post a Comment