Tuesday, June 7, 2011

MWAKILISHI MSAIDIZI WA THE GUARDIAN IRINGA AFARIKI DUNIA

MFANYAKAZI wa Kampuni ya The Guardian Ltd Mkoani Iringa, Isdory Fungo (41) amefariki dunia.
Fungo alifariki dunia alfajiri ya Juni 07,mwaka huu katika hospitali ya Wilaya ya Makete alikokimbizwa baada ya hali yake kubadilika ghafla.
Taarifa iliyotolewa na Mwakilishi wa Kampuni ya The Guardian Mkoa wa Iringa, Kishede Msuya imesema awali, Fungo alikuwa anaugua malaria na miguu ambapo alipata matibabu Mjini Iringa kabla ya kwenda hospiatli ya Misheni ya Ikonda wilayani Makete kwa matibabu zaidi ambako alilazwa kwa wiki moja na kurejea kwa kaka yake Mjini Makete.
Hata hivyo,akiwa nyumbani kwa kaka yake usiku wa kuamkia jana hali yake ilibadilika ghafla ambapo alikimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Makete lakini alifariki dunia muda mfupi baadaye.
Kampuni ya The Guardian inaungana na wafiwa katika msiba huo, ambao marehemu Isdory atazikwa nyumbani kwao Makete.
Kabla ya kuajiriwa na kampuni ya The Guardian mwaka 2008 alikuwa wakala wa magazeti ya kampuni mbalimbali katika kituo cha Makambako wilayani Njombe,kazi ambayo aliifanya kwa zaidi ya miaka 10.
Hadi kifo chake hapo jana,Fungo alikuwa Mwakilishi Msaidizi wa Mkoa wa Iringa wa kampuni ya The Guardian Ltd. Marehemu ameacha mjane na mtoto mmoja.

No comments:

Post a Comment