Saturday, November 27, 2010

CHUO KIKUU KISHIRIKI CHA ELIMU MKWAWA TAABANI

CHUO Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) cha Mkoani Iringa, kina majukumu makubwa ya kitaifa ambayo ni pamoja na kusaidia au kuchangia upanuzi wa elimu nchini.

Chuo hiki kimepewa heshima kubwa na Taifa ya kuhakikisha kuwa kinawaandaa walimu wenye sifa sitahiki kutekeleza yale yanayotarajiwa na Taifa. Kinatakiwa kuwaandaa wanafunzi wake kwa ajili ya ulimwengu ujao wa ajira,ulimwengu wa utandawazi na ushindani mkubwa.

Chuo hiki ni muhimu kwa sababu kinasaidia kuondosha tatizo kubwa na la muda mrefu la upungufu wa walimu wenye shahada linaloikabili Taifa kwa muda mrefu.

Hata hivyo,licha ya majukumu haya mazito ya kitaifa,Chuo Kikuu cha Mkwawa kinakabiliwa na changamoto nyingi kiasi kwamba baadhi ya wanafunzi wa mwanzo kusoma hapo, Chuo hicho kilipoanza rasmi mwaka 2005/2006 walifikia hatua ya kudai kuwa Serikali imewapeleka pale ili kuwatunuku shahada za majaribio kwa madai kuwa walikuwa wanasoma katika mazingira magumu mno yasiyostahili kuitwa Chuo Kikuu.

Kuanzishwa kwa MUCE:

Chuo Kikuu cha Mkwawa kilianzishwa rasmi mwaka 2005 baada ya iliyokuwa shule ya sekondari ya Mkwawa (Mkwawa High School) kuvunjwa na wanafunzi waliokuwa hapo kuhamishiwa katika shule za sekondari za Ifunda na Songea Girls.

Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa sambamba na Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Changómbe vilianzishwa ili kukabiliana na tatizo kubwa la uhaba wa walimu wenye shahada wa shule za sekondari nchini baada ya Serikali kufanikiwa sana kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM).

Wanafunzi wengi walikuwa wanakwenda shule za sekondari lakini changamoto kubwa ikawa ni vyumba vya madarasa katika shule za sekondari pamoja na walimu wa shule hizo.

Wakati Serikali ikianzisha Mpango wa Maendeleo ya shule za Sekondari (MMES) ili kukabiliana na tatizo la madarasa na majengo ya sekondari kwa jumla, iliona pia kuna haja ya kwenda sambamba na utatuaji wa tatizo au changamoto ya upungufu wa walimu wenye shahada wa shule za sekondari nchini, ndipo wazo likaja la kufunga shule za sekondari Mkwawa na Chuo cha ufundi Chang´ombe ili maeneo hayo yapandishwe hadhi na kuwa Vyuo vikuu vishiriki vya elimu vya Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam.

Changamoto zinazoikabili MUCE:

Wakati kinaanza rasmi,mwaka 2006/2007 Chuo Kikuu cha Mkwawa kilidahili wanafunzi 1,176. Licha ya ukarabati mdogo uliokuwa umefanyika, wanafunzi hao pamoja na wahadhiri wa Chuo hicho,kwa sehemu kubwa walilazimika kutumia miundombinu iliyorithiwa kutoka shule ya sekondari ya Mkwawa.

Udahili wa wanafunzi katika Chuo hicho umeendelea kuongezeka mwaka na hata mwaka ambapo mwaka 2007/2008 kilidahili wanafunzi 846, mwaka 2008/2009 wanafunzi 654, mwaka 2009/2010 wanafunzi 822 na mwaka huu, yaani 2010/2011 wamedahiliwa wanafunzi 878.

Licha ya ongezeko hilo la wanafunzi,miuondombinu ya Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa imeendelea kuwa haikidhi mahitaji ya wanafunzi na wahadhiri.

Katika hali isiyo ya kawaida, katika mahafali ya pili ya MUCE yaliyoafanyika Novemba 20,mwaka huu, wazungumzaji wote katika sherehe za mahafali hayo walijikita zaidi kulalamikia matatizo au changamoto zinazoikibili Chuo hicho, malalamiko kama hayo, mara nyingi kusema kweli yanasikika zaidi katika shule za sekondari hususan za Kata.

Katika mahafali hayo,wanafunzi 677 kati yao wanawake 181 walitunukiwa shahada katika fani nne ambazo ni shahada ya Elimu ya Jamii na Ualimu (481) shahada ya Elimu katika Sayansi za Jamii (102), shahada ya Sayansi na Ualimu (74) na shahada ya Elimu katika Sayansi (20).

Akizungumza katika mahafali hayo,Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam,Professa Rwekaza Mukandala alisema ni wazi kuwa mafunzo bora yanahitaji uboreshaji miundombinu pamoja na rasilimali nyingine zinazohitajika katika kuwaandaa vyema wanafunzi.

“Chuo kinathamini misaada yote inayoendelea kutolewa na serikali ili kuhakikisha kuwa mazingira ya Chuo ni wezeshaji kwa ufundishaji,utafiti na huduma kwa jamii. Mchango wa serikali utaweza kuhakikisha kuwa mahitaji muhimu kwa mafunzo ikiwa ni pamoja na kumbi za mihadhara,madarasa,maabara,maktaba,zana mbalimbali za masomo na mahitaji mengine vinapatikana,” anasema Professa Mukandala.

Professa Mukandala alisema kuwa wakati Chuo kinatambua mchango mkubwa wa serikali,kwa upande mwingine msaada unaotolewa umekuwa kidogo ikilinganishwa na mahitaji halisi na mipango ya Chuo.

“Kwa mfano,kutokana na uhaba huu, wakati ambabo matarajio ya Chuo yalikuwa ni kudahili wanafunzi 1,000 katika mwaka wa masomo 2009/2010 na wanafunzi 1,300 katika mwaka wa masomo 2010/2011,Chuo kimefanikiwa kudahili wanafunzi 800 na 878 tu katika miaka hiyo ya masomo na hii imetokana na uwezo mdogo wa miundombinu iliyopo Chuoni ikiwa ni pamoja na rasilimali nyingine husianifu za watu,” anaongeza Professa Mukandala.

Naye Mkuu wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa,Professa Phillemon Mushi anasema kwa upande wa malazi ya wanafunzi,Chuo bado kina nafasi 1,100 tu katika mabweni yaliyopo hivyo wanafunzi 737 sawa na asilimia 40.2 wanakaa nje ya Chuo ambapo hakuna uhakika wa mazingira muafaka ya kuweza kufanya kazi zao kama wale ambao wako ndani ya mabweni ya Chuo.

“Hili ni mojawapo ya mambo yanayoweza kuchangia wanafunzi kutofanya vizuri kama ambavyo wangeweza kama mazingira yangekuwa yanakubalika,” alisema Professa Mushi na kuongeza:

“Inaeleweka kuwa katika nchi nyingi suala la mabweni sio kipaumbele kwa Vyuo, ila hapa Tanznania na hususan hapa Iringa ni kipaumbele kwa sababu nje ya Chuo Kikuu cha Mkwawa hakuna nyumba za kutosha zinazofaa kwa malazi ya wanafunzi, ombi letu ni kwamba serikali ikiwezeshe Chuo au wawekezaji kujenga mabweni”.

“Changamoto kubwa katika shughuli za Chuo ni jinsi ya kupanua miundombinu, kwa mfano,maktaba iliyopo pamoja na ukarabati mkubwa uliofanywa, bado ni ndogo sana kukidhi mahitaji ya wanafunzi na wahadhiri,” alisema Professa Mushi.

Alisema pia kuwa Chuo hicho kinachangamoto ya kuongeza au kuendeleza rasilimali watu kwani kwa sasa Chuo hicho kina wanataaluma 136 na kati ya hao,kumi tu ndiyo wana shahada ya udhamivu (PhD), 35 wana shahada ya udhamili na 91 wana shahada ya kwanza.

“Kwa kawaida wanataaluma wote wanaofundisha Chuo Kikuu wanatakiwa wawe na shada ya udhamivu,” aliongeza Professa Mushi.

Kufuatia hali hiyo,Professa Mushi alisema Chuo hicho kimekuwa kikiendesha shughuli zake kwa kuajiri wahadhiri wa muda wengi wao kutoka kampasi ya Mlimani ambapo mwaka jana pekee,wahadhiri wa muda walioajiriwa ni 147 na kukigharimu Chuo hicho zaidi ya Sh.milioni 600 fedha ambazo ni zaidi ya nusu ya fedha za matumizi mengineyo (OC) ya Chuo hicho.

Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam,Jaji Joseph Warioba naye hakuwa na jingine zaidi ya kulalamikia miundombinu mibovu ya Chuo hicho cha Mkwawa ambaye aliiomba serikali kuongeza fungu la fedha la kusomesha wahadhiri katika Chuo Kikuu cha Mkwawa.

Jaji Warioba alisema ikiwezekana, ni vyema serikali ikabuni mpango mahsusi wa kusomesha wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Mkwawa katika ngazi ya udhamili na udhamivu.

Jaji Warioba hata hivyo, aliipongeza serikali kwa kuanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu (MMEJU) Mpango ambao alisema utaiwezesha sekta ya elimu ya juu kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Mikakati ya MUCE kukabiliana na Changamoto zake:

Kutokana na uchanga wa Chuo Kikuu cha Mkwawa na mazingira magumu wakati kilipoanzishwa, kumekuwepo na mikakati ya kukifanya kiwe na nyenzo zote za kutoa elimu bora ambapo imeanzishwa miradi mbalimbali ambayo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo la utawala,ofisi,kumbi za mihadhara na maabara za sayansi.

Mradi mwingine ni wa kuendeleza rasilimali watu, mwingine wa kupanua maktaba. Upo pia mradi wa kuongeza nafasi na idadi ya ofisi kwa ajili ya wafanyakazi, kuboresha mabweni ya wanafunzi, kukarabati miundombinu na mifumo ya maji, barabara,umeme,mawasiliano na kuboresha mazingira ya chuo.

No comments:

Post a Comment