McEddy Elroy

Monday, February 7, 2011

AWAMU ya kwanza ya upanuzi wa hospitali ya Mkoa wa Iringa, inatarajiwa kukamilika mwisho mwa mwezi ujao, yaani Machi, mwaka huu.

Upanuzi huo unaogharimiwa na hospitali rafiki na hospitali hiyo kutoka nchini Italia ya Vicenza,unagharimu fedha za kitanzania,Sh.bilioni mbili.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Iringa,Dk.Oscar Gabone amesema upanuzi huo unajumuisha ujenzi wa jengo la kujifungulia kina mama litakalokuwa na vitanda 20.

Katika upanuzi huo, limo pia jengo la upasuaji kina mama wajawazito na jengo laghorofa moja la wodi ya watoto litakalokuwa na vitanda 100.

Aidha,licha ujenzi wa majengo, msaada huo pia unajumuisha samani zote za majengo hayo na vifaa vya kisasa vya tiba pamoja na mafunzo ya namna bora ya kuhudumia kina mama na watoto yatakayotolewa kwa wafanyakazi watakaokuwa wanahudumu kwenye majengo hayo.

Hospitali hiyo ya Visenza ya nchini Italia imesaini mkataba na hospitali ya rufaa ya KCMC wa kutoa mafunzo ya namna bora ya kuhudumia kina mama na watoto kwa baadhi ya watumishi wa hospitali ya Mkoa wa Iringa.

Kwa mujibu wa Dk.Gabone,majengo yatakayokamilika Machi 31,mwaka huu, ni jengo la kujifungulia kina mama na jengo la upasuaji kina mama wajawazito hali ambayo itafanya huduma za kina mama wajawazito kuimarika na kuwa bora zaidi hospitalini hapo.

”Nina imani kwamba baada ya upanuzi huu kukamilika huduma katika hospitali yetu (ya Mkoa wa Iringa) hususani kwa kina mama wajawazito na watoto zitakuwa bora sana kwa sababu marafiki zetu wa Italia watatupatia Elimu, Majengo bora, eneo safi la kutolea huduma na vifaa vya kisasa kabisa,” alisema Dk.Gabone.

No comments:

Post a Comment