McEddy Elroy

Saturday, February 5, 2011

UFISADI WATIKISA CHUO KIKUU CHA ELIMU MKWAWA

UONGOZI wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce) cha Mkoani Iringa, unakabiliwa na tuhuma nzito za kufanya ufisadi wa aina mbalimbali chuoni hapo.

Ufisadi unaodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa chuo hicho ni pamoja na wizi wa fedha za Chuo hicho kupitia mikataba ya wazabuni, upendeleo, kujilipa mishahara mara mbili pamoja na kuendesha akaunti za benki za muda maalum (Fixed Deposit Account) kwa kutumia fedha za serikali au za wafadhili na hivyo kuchelewesha malipo mbalimbali ya watoa huduma na kwa wanafunzi.

Uongozi wa Chuo hicho umethibitisha baadhi ya madai na kuyakanusha vikali mengine huku ukidai kuwa ni njama za baadhi ya watu au wafanyakazi wanaotaka kuchafua taswira ya taasisi hiyo ya elimu ya Juu.

Uchunguzi wa zaidi ya wiki mbili umebaini kuwa kuna wafanyakazi watatu (majina yao tunayo) wa Chuo hicho ambao wamekuwa wakijilipa mishahara mara mbili.

Nyaraka zinaonesha kuwa mfanyakazi mmoja ambaye ngazi ya mshahara wake ni kati ya Sh 318,620/- na 339,860/- lakini kwa kupendelewa au kwa wizi tu amekuwa akilipwa mshahara wa Sh.750,000/- toka Agosti 2006 alipoajiriwa.

Mwingine ambaye mshahara wake ni Sh.622,578 /-amekuwa akijilipa au kulipwa mshahara huo pamoja na mshahara mwingine wa Sh.700,000/- kila mwezi.

Mfanyakazi huyo hulipwa mishahara hiyo kwa ustadi mkubwa kwa kupitia akaunti za Chuo hicho za benki mbili tofauti.

Aidha, uchunguzi unaonesha kuwa mfanyakazi wa tatu ambaye tayari amekwisha acha kazi Muce, licha ya kuwa mshahara wake ulikuwa wa Sh.911,060/- pia alikuwa akichota mshahara mwingine wa Sh.507,590/- kupitia akaunti ya benki nyingine.

Aidha, tumeshindwa kuwataja wafanyakazi hao kwa majina kutokana na kushindwa kuwapata ili kutoa upande wao kwa kuwa mmoja yuko Tanga likizo, mwingine kaacha kazi hivi karibuni kwa notisi fupi na mwingine yuko rumande akikabiliwa na kesi nyingine.

Hata hivyo, kuhusu madai hayo ya kulipana mishahara mara mbili,Mkuu wa Chuo hicho,Professa Phillemon Mushi alikiri kuwabaini watuhumiwa hao na kueleza kuwa hatua zimekwishachukuliwa dhidi yao.

Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kuwa watuhumiwa hao hawajachukuliwa hatua za kisheria zaidi ya kuondolewa katika idara walizokuwepo na kuhamishiwa idara tofauti.

Madai mengine yanayoukabili uongozi wa Chuo hicho ni wizi wa fedha za umma kupitia mikataba ya mzabuni aliyekuwa akitoa huduma moja Chuoni hapo.

Taarifa zinaonesha kuwa, kulingana na mkataba wake, malipo ya mzabuni huyo kwa mwezi ilikuwa ni dola za kimarekani 13,040/- lakini baadhi ya watumishi wa idara ya uhasibu na ugavi walikuwa wakishirikiana kulipa mara mbili kiasi hicho cha fedha.

Wizi huo ulikuwa unafanikishwa kwa ustadi mkubwa kwa kuandika hundi mbili zenye kiasi cha dola za kimarekani 13,040/- (19,951,200) kwa kila hundi huku zikionesha kuwa anayelipwa ni mzabuni huyo na kwamba wizi huo unadaiwa kufanyika kati ya mwaka 2006/2007 na 2008/2009.

”Lakini baada ya hundi hizo kuwa zimepita kila mahali kwa ajili ya kuidhinishwa, hundi moja ilikuwa inawekwa kwenye akaunti tofauti na wafanyakazi hao kugawana fedha hizo,” anasema mtoa taarifa wetu.

Nipashe imefanikiwa kupata namba za hundi na akaunti iliyokuwa inatumika kufanikisha wizi huo.

Hata hivyo,Professa Mushi alipoulizwa juu ya suala hilo alisema ni jambo la zamani (anataja mwaka 2009) na kwamba kwa sasa hilo siyo jambo la kujadiliwa.

”Jamani hebu mtuache nasi tufanye kazi basi hata kidogo hiyo Issue ni ya zamani mno, hata huyo (anataja jina la mzabuni) hayupo tena hapa chuoni,” alisema Professa Mushi.

”Unajua inaonekana mmeiba taarifa ya ukaguzi ambayo hata haikuwa imekamilika na ilikuwa siri, huyo mtu anayekuletea mambo hayo anatapatapa tu”, aliongeza Professa Mushi kwa ukali.

Aidha, yapo madai ya Chuo hicho kuendesha akaunti za muda maalum bila kuweka wazi faida inayotokana na akaunti hizo.

Uchunguzi unaonesha kuwa,mpaka Juni,mwaka jana, Chuo hicho kilikuwa kinaendesha akaunti zaidi ya nne za muda maalum ambazo zilikuwa na zaidi ya Sh.milioni 500.

Akaunti nne ambazo zipo kwenye benki moja yenye tawi mjini Iringa zinaonesha kuwa moja ilikuwa na kiasi cha Shilingi za kitanzania 10,090,999.55, inayofuata ilikuwa na Sh.201,247,671.23, pia ilikuwepo akaunti yenye Sh.252,853,107.40 na nyingine ilikuwa na Sh.75,195,042.70 ambapo jumla yake ni Sh.milioni 539,386,820.88.

Hata hivyo, awali alipohojiwa,Professa Mushi alisema aulizwe Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho (Fedha na Utawala),Professa Machiwa kwa maelezo kuwa ndiye alikuwa anafahamu vyema.

Professa Machiwa alipohojiwa alidai kuwa akaunti hizo hazikuwa kwenye orodha ya akaunti za Chuo hicho na kwamba hakuwa anazifahamu wala kuwa na taarifa nazo.

”Hata nikikuonyesha taarifa yangu ya kila siku akaunti hizo hazimo labda kamwone mhasibu wa Chuo anaweza kuwa anataarifa zaidi,” alisema Professa Machiwa lakini kabla mwandishi hajaondoka akaamua vinginevyo:

”Hebu ngoja nimpigie mhasibu aende Benki naye akaangalie ili atuletee taarifa kama akaunti hizo ni za Mkwawa University, kwa hiyo njoo baadaye nitakupa taarifa”. Alisema.

Hata hivyo, mwandishi aliporejea Mchana wa Januari 28,mwaka huu, Professa Machiwa alisema watu wa benki walikuwa wamegoma kutoa taarifa za akaunti hizo mpaka waandikiwe barua.

”Nimeandika barua nimeshawapelekea hivyo naomba uje wiki ijayo, na kwa kuwa sitakuwepo, utakuta taarifa kwa Katibu Muhtasi wangu,” alisema .

Mwandishi wa blog hii alifuatilia kwa siku tatu mfululizo bila kupata majibu kwa Katibu Muhtasi wake na kuamua kumtafuta Professa Mushi kwa simu ambaye baada ya kuulizwa suala hilo alisema:

”Mbona Professa Machiwa ameshakujibu, usinisumbue,” alisema kwa kifupi na kukata simu.

Hata hivyo, baadaye alipiga simu tena kwa mwandishi na kueleza kuzifahamu akaunti hizo na kudai kuwa akaunti hizo zilikuwa za zamani na kwamba hivi sasa hazipo tena.

”Unaziona kama ni nyingi lakini akaunti ni moja tu yaani kila akaunti ya kwanza inapokuwa tayari faida inachukuliwa na kufunguliwa akaunti nyingine,” alisema.

Professa Mushi alifafanua kuwa fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti ya muda maalum zilitoka kwa wafadhili ambao hata hivyo hakuwataja, ambazo zilikuwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo lakini baada ya mkandarasi kusuasua,waliamua kuziweka kwenye akaunti ya muda maalum ili kuepusha kuzitumia kwa shughuli zingine.

No comments:

Post a Comment