McEddy Elroy

Thursday, March 10, 2011

MWAKALEBELA AIGARAGAZA TAKUKURU MAHAKAMANI KWA MARA YA PILI

MAHAKAMA ya Mkoa wa Iringa,kwa mara nyingine imemwachia huru aliyekuwa mshindi wa kwanza katika kura za maoni nafasi ya ubunge wa Iringa Mjini (CCM),Frederick Mwakalebela (41) na mkewe Selina katika kesi namba nane ya kutoa hongo kwenye mchakato wa kura za maoni iliyokuwa inawakabili.
Mwakalebela pia aliachiwa huru Februari 25,mwka huu na hakimu Festo Lwila wa mahakama ya wilaya ya Iringa kwenye kesi namba 4 iliyokuwa inamkabili peke yake baada ya hakimu huyo kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulikuwa haujatenda haki kuchanganya makosa mawili kwenye shtaka moja na kusema kuwa upande wa mashtaka ulikuwa na hiari ya kumshtaki tena mahakamani Mwakalebela kama wanaona inafaa kufanya hivyo lakini kwa kutumia kosa moja na sheria moja kati ya mbili walizokuwa wametumia.
Tofauti na kesi namba nne,Mahakama ya Mkoa wa Iringa chini ya hakimu wa mahakama hiyo,Mary Senapee amemwachia huru Mwakalebela na Mkewe Selina baada ya kuridhika na hoja kuu mbili za utetezi uliokuwa unaongozwa na Bsil Mkwatta wa Mkwatta Law Chambers.
Hoja hizo ni kwamba upande wa mashtaka wakati wanapeleka hati ya mashtaka mahakamani ilipindi waonyeshe wazi kwamba Mwakalebela na Mkewe walitoa hongo kwa ajili ya kutaka upendeleo au kupindisha utaratibu wa kawaida kwa niaba ya ofisi yao au mkubwa wao na kwamba waliopokea pia walifanya hivyo kwa niaba ya ofisi zao,biashara zao au mkubwa wao (In relation to his principal affairs or Business).
Kwamba kifungu namba 15(1)(b) cha sheria ya kuzuia na kupammbana na rushwa ya mwaka 2007 kinawahusu watumishi wa serikali au wanaoshikilia ofisi za umma hivyo ni lazima hati ya mashitaka ionyeshe waziwazi maneno hayo.
Hoja ya pili aliyokubaliana nayo ni upande wa mashtaka kutotenda haki kwa kuchanganya makosa mawili kwenye shtaka moja kwa kutumia sheria mbili tofauti – sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya Gharama za uchaguzi ya mwaka 2010.
Katika hoja ya kwanza Mwendesha mashtaka wa Takukuru Mkoa wa Iringa,Imani Nitume alisema maneno hayo siyo lazima yaonyeshwe kwenye hati ya mashtaka kwani yanaweza kusubiri wakati wa ushahidi.
Hata hivyo,hakimu Senapee alijiridhisha kuwa hoja hizo zina nguvu kisheria na kwamba kuchanganya makosa mawili kwenye shtaka moja si haki pia mahakama haiwezi kusubiri ushahidi ili kujua Mwakalebela na Mkewe pamoja na waliopokea hongo hiyo walikuwa na ´Principals´ wakati wa kutenda kosa hilo hivyo akawachia huru watuhumiwa na kueleza kuwa upande wa mashtaka wanayo haki ya kukata rufaa kama hawajaridhika na hukumu hiyo.
Mwakalebela kwa pamoja na mkewe Selina,wanadaiwa kuwa mnamo mwezi Juni mwaka jana, katika kijiji cha Mkoga Manispaa ya Iringa, walitoa hongo ya Sh.100,000 kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamisi Luhanga ili azigawe kwa wapiga kura 30 wa CCM ili wampigie kura za maoni zilizofanyika Agosti mosi, mwaka jana.

No comments:

Post a Comment