McEddy Elroy

Thursday, March 10, 2011

POLISI WADAIWA KUJERUHI MWANAFUNZI KWA KIPIGO

JESHI la Polisi mkoani hapa, limetupiwa tuhuma ya kumjeruhi kwa kipigo mwanafunzi wa kidato cha nne wa sekondari ya Efatha iliypo Kitwiru Manispaa ya Iringa wakati wakijaribu kuwatawanya wanafunzi hao Machi 9.

Taarifa za kujeruhiwa kwa mwanafunzi huyo zimetolewa kwa Mbunge wa viti maalum (CCM) Mkoa wa Iringa,Ritha Kabati ambaye alitembela shule hiyo machi 10,mwaka huu kujua tatizo pamoja na kuwa pole wanafunzi.

Mkuu wa shule hiyo,Kenneth Ngelangela alimwambia Mbunge huyo aliyekuwa ameongozana na Meya wa Manispaa ya Iringa,Mstahiki Aman Mwamwindi kuwa mwanafunzi alijeruhiwa kwa kipigo cha polisi ni Giveness Mvamba.

Aidha,Mkurugenzi wa shule hiyo Paul Tabani alisema mwanafunzi huyo alikuwa anauguza majeraha yake nyumbani na kwamba jana walikuwa wanaangalia utaratibu wa kumpeleka hospitali kwa matibabu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,Claus Mwasyeba alisema hana taarifa kama kuna mwanafunzi alijeruhiwa na kuomba kama mwanafunzi huyo yupo basi aende ofisini kwake akamwone.

Katika vurugu hizo, alisema hakuna mwanafunzi aliyekamatwa wala kuhojiwa lakini tyaarifa zilizotolewa kwa mbunge huyo zilieleza kuwa baadhi ya wanafunzi hususani wa kike walikamatwa na kutupwa kwenye magari ya polisi kitendo ambacho Mbunge huyo aliunga mkono kwa maelezo kuwa aliwaona wanafunzi hao wakiwa kwenye magari ya polisi kwenye picha za taarifa ya habari ya juzi usiku ya kituo cha ITV.

Vurugu hizo zilizuka juzi asubuhi baada ya wanafunzi hao kuwaweka kiti moto wakaguzi wa shule kanda ya nyanda za juu kusini wakitaka kujua uhalali wa kuzuiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha pili, iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na NIPASHE walisema kuwa, vulumai hiyo ilianza baada ya mmoja wa wakaguzi hao Benadetha Mtitu kuwapa majibu ya hovyo, pale walipotaka kujua sababu za kuzuiwa matokeo ya mitihani yao wakati walitimiza masharti yote ya mitihani hiyo.

“Alituambia ni bora tukalime na wasichana waende kuolewa kwa sababu walikuwa wanapoteza muda bure shuleni hapo kwa kuwa shule hiyo ilikuwa haijatimiza masharti kadhaa,” alidai mwanafunzi wa kidato cha nne,Shamte Mussa wakati akimkariri mkaguzi huyo.

Wanafunzi 500 wa kidato cha pili walifanya mitihani yao baada ya kulipa gharama za mitihani lakini hadi sasa wahawajapatiwa matokeo yao jambo ambalo liliwalazimu kuhoji kama kanuni haziruhusu wanafunzi zaidi ya 80 katika mkondo mmoja kufanya mitihani hiyo kwa nini ofisi ya elimu ilichukua fedha zao na kuwaruhusu wanafunzi wote 500 kufanya mitihani hiyo kisha kuzuia matokeo yao.

Akizungumza shuleni hapo Mbunge Kabati kwanza aliwapa pole wanafunzi hao kwa kuzuiliwa matokeo yao lakini akawataka kuwa watulivu na waendelee kusoma na kwamba yeye binafsi atalifikisha suala hilo kwa Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi.

Kwa upande wake,mkaguzi anayedaiwa kuwatukana wanafunzi hao,Benadetha Mtitu hakupatikana jana lakini Mkuu wa Ukaguzi wa shule Kanda ya Nyanda za juu Kusini,Hebron Mlelwa alikataa kataka kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa limeshafika Wizara ya Eilumu na kwamba yeye si msemaji wa Wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment