McEddy Elroy

Sunday, March 27, 2011

WATU WANAONIFUATILIA WAIBA LAPTOP YANGU

Habari ndugu wapenzi wa Blog hii muipendayo.
Nasikitika kutoa taarifa kwamba,watu wasiofahamika wameingia ofisini kwangu kwa kutumia Master Keys na kuiba Computer yangu ndogo aina ya Apple na sasa imekuwa ngumu kuwa hewani mara kwa mara kwa sababu ya tatizo hilo.

Hizi huu umenistua sana hususani ikizingatiwa kwamba, wameingia na kuchukua Laptop tu hali inayonipa mashaka kama kweli walikuwa wanatafuta hiyo Laptop au wanatafuta kilichomo kwenye Laptop hiyo.

Pale mezani ilipokuwa Laptop,kulikuiwepo vitu vingi vyenye thamani kubwa kama Mordem ya Internet,Dvcam Camera yenye thamani ya dola za kimarekani 4,000, simu ya mkononi aina ya Nokia ambayo hata hivyo ni mbovu kidogo na ndiyo maana ilikuwa inabaki ofisini,kulikuwa pia na flash mbili moja ya GB mbili na nyingine ya MB 250 na vitu vingine vingi vidogo vidogo ambavyo nina uhakika kama ni vibaka wa kawaida wangevikusanya!.

Nashawishika kuamini kwamba kuna watu walikuwa wananifuatilia hasa baada ya kuwa nimeanza kuichunguza taasisi moja kubwa hapa mkoani Iringa ambayo baadhi ya viongozi na watumishi wake wana tuhuma nzito za ubadhilifu wa fedha za umma.

Nimetoa taarifa Polisi na kupewa RB Na.IR/RB/1666/2011 ya Machi 25,mwaka huu.Naomba dua zenu ili niweze kuipata Computer hiyo na kama kuna watu wananifuatilia, basi wasifanikiwe kunidhuru.

Hata hivyo,nawaahidi wapenzi wangu kwamba pamoja na tatizo hili nitaendelea kuwaletea vitu mlivyozoea hususani taarifa za uchunguzi bila woga wala upendeleo.

Tuko pamoja.!

Thursday, March 10, 2011

POLISI WADAIWA KUJERUHI MWANAFUNZI KWA KIPIGO

JESHI la Polisi mkoani hapa, limetupiwa tuhuma ya kumjeruhi kwa kipigo mwanafunzi wa kidato cha nne wa sekondari ya Efatha iliypo Kitwiru Manispaa ya Iringa wakati wakijaribu kuwatawanya wanafunzi hao Machi 9.

Taarifa za kujeruhiwa kwa mwanafunzi huyo zimetolewa kwa Mbunge wa viti maalum (CCM) Mkoa wa Iringa,Ritha Kabati ambaye alitembela shule hiyo machi 10,mwaka huu kujua tatizo pamoja na kuwa pole wanafunzi.

Mkuu wa shule hiyo,Kenneth Ngelangela alimwambia Mbunge huyo aliyekuwa ameongozana na Meya wa Manispaa ya Iringa,Mstahiki Aman Mwamwindi kuwa mwanafunzi alijeruhiwa kwa kipigo cha polisi ni Giveness Mvamba.

Aidha,Mkurugenzi wa shule hiyo Paul Tabani alisema mwanafunzi huyo alikuwa anauguza majeraha yake nyumbani na kwamba jana walikuwa wanaangalia utaratibu wa kumpeleka hospitali kwa matibabu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,Claus Mwasyeba alisema hana taarifa kama kuna mwanafunzi alijeruhiwa na kuomba kama mwanafunzi huyo yupo basi aende ofisini kwake akamwone.

Katika vurugu hizo, alisema hakuna mwanafunzi aliyekamatwa wala kuhojiwa lakini tyaarifa zilizotolewa kwa mbunge huyo zilieleza kuwa baadhi ya wanafunzi hususani wa kike walikamatwa na kutupwa kwenye magari ya polisi kitendo ambacho Mbunge huyo aliunga mkono kwa maelezo kuwa aliwaona wanafunzi hao wakiwa kwenye magari ya polisi kwenye picha za taarifa ya habari ya juzi usiku ya kituo cha ITV.

Vurugu hizo zilizuka juzi asubuhi baada ya wanafunzi hao kuwaweka kiti moto wakaguzi wa shule kanda ya nyanda za juu kusini wakitaka kujua uhalali wa kuzuiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha pili, iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na NIPASHE walisema kuwa, vulumai hiyo ilianza baada ya mmoja wa wakaguzi hao Benadetha Mtitu kuwapa majibu ya hovyo, pale walipotaka kujua sababu za kuzuiwa matokeo ya mitihani yao wakati walitimiza masharti yote ya mitihani hiyo.

“Alituambia ni bora tukalime na wasichana waende kuolewa kwa sababu walikuwa wanapoteza muda bure shuleni hapo kwa kuwa shule hiyo ilikuwa haijatimiza masharti kadhaa,” alidai mwanafunzi wa kidato cha nne,Shamte Mussa wakati akimkariri mkaguzi huyo.

Wanafunzi 500 wa kidato cha pili walifanya mitihani yao baada ya kulipa gharama za mitihani lakini hadi sasa wahawajapatiwa matokeo yao jambo ambalo liliwalazimu kuhoji kama kanuni haziruhusu wanafunzi zaidi ya 80 katika mkondo mmoja kufanya mitihani hiyo kwa nini ofisi ya elimu ilichukua fedha zao na kuwaruhusu wanafunzi wote 500 kufanya mitihani hiyo kisha kuzuia matokeo yao.

Akizungumza shuleni hapo Mbunge Kabati kwanza aliwapa pole wanafunzi hao kwa kuzuiliwa matokeo yao lakini akawataka kuwa watulivu na waendelee kusoma na kwamba yeye binafsi atalifikisha suala hilo kwa Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi.

Kwa upande wake,mkaguzi anayedaiwa kuwatukana wanafunzi hao,Benadetha Mtitu hakupatikana jana lakini Mkuu wa Ukaguzi wa shule Kanda ya Nyanda za juu Kusini,Hebron Mlelwa alikataa kataka kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa limeshafika Wizara ya Eilumu na kwamba yeye si msemaji wa Wizara hiyo.

MWAKALEBELA AIGARAGAZA TAKUKURU MAHAKAMANI KWA MARA YA PILI

MAHAKAMA ya Mkoa wa Iringa,kwa mara nyingine imemwachia huru aliyekuwa mshindi wa kwanza katika kura za maoni nafasi ya ubunge wa Iringa Mjini (CCM),Frederick Mwakalebela (41) na mkewe Selina katika kesi namba nane ya kutoa hongo kwenye mchakato wa kura za maoni iliyokuwa inawakabili.
Mwakalebela pia aliachiwa huru Februari 25,mwka huu na hakimu Festo Lwila wa mahakama ya wilaya ya Iringa kwenye kesi namba 4 iliyokuwa inamkabili peke yake baada ya hakimu huyo kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulikuwa haujatenda haki kuchanganya makosa mawili kwenye shtaka moja na kusema kuwa upande wa mashtaka ulikuwa na hiari ya kumshtaki tena mahakamani Mwakalebela kama wanaona inafaa kufanya hivyo lakini kwa kutumia kosa moja na sheria moja kati ya mbili walizokuwa wametumia.
Tofauti na kesi namba nne,Mahakama ya Mkoa wa Iringa chini ya hakimu wa mahakama hiyo,Mary Senapee amemwachia huru Mwakalebela na Mkewe Selina baada ya kuridhika na hoja kuu mbili za utetezi uliokuwa unaongozwa na Bsil Mkwatta wa Mkwatta Law Chambers.
Hoja hizo ni kwamba upande wa mashtaka wakati wanapeleka hati ya mashtaka mahakamani ilipindi waonyeshe wazi kwamba Mwakalebela na Mkewe walitoa hongo kwa ajili ya kutaka upendeleo au kupindisha utaratibu wa kawaida kwa niaba ya ofisi yao au mkubwa wao na kwamba waliopokea pia walifanya hivyo kwa niaba ya ofisi zao,biashara zao au mkubwa wao (In relation to his principal affairs or Business).
Kwamba kifungu namba 15(1)(b) cha sheria ya kuzuia na kupammbana na rushwa ya mwaka 2007 kinawahusu watumishi wa serikali au wanaoshikilia ofisi za umma hivyo ni lazima hati ya mashitaka ionyeshe waziwazi maneno hayo.
Hoja ya pili aliyokubaliana nayo ni upande wa mashtaka kutotenda haki kwa kuchanganya makosa mawili kwenye shtaka moja kwa kutumia sheria mbili tofauti – sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya Gharama za uchaguzi ya mwaka 2010.
Katika hoja ya kwanza Mwendesha mashtaka wa Takukuru Mkoa wa Iringa,Imani Nitume alisema maneno hayo siyo lazima yaonyeshwe kwenye hati ya mashtaka kwani yanaweza kusubiri wakati wa ushahidi.
Hata hivyo,hakimu Senapee alijiridhisha kuwa hoja hizo zina nguvu kisheria na kwamba kuchanganya makosa mawili kwenye shtaka moja si haki pia mahakama haiwezi kusubiri ushahidi ili kujua Mwakalebela na Mkewe pamoja na waliopokea hongo hiyo walikuwa na ´Principals´ wakati wa kutenda kosa hilo hivyo akawachia huru watuhumiwa na kueleza kuwa upande wa mashtaka wanayo haki ya kukata rufaa kama hawajaridhika na hukumu hiyo.
Mwakalebela kwa pamoja na mkewe Selina,wanadaiwa kuwa mnamo mwezi Juni mwaka jana, katika kijiji cha Mkoga Manispaa ya Iringa, walitoa hongo ya Sh.100,000 kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamisi Luhanga ili azigawe kwa wapiga kura 30 wa CCM ili wampigie kura za maoni zilizofanyika Agosti mosi, mwaka jana.